Utafiti maendeleo ya elimu ya msingi waja

Mkurugenzi wa Mafunzo  ya Elimu ya Juu kutoka wizara hiyo, Profesa  Sylvia Temu amesema utafiti huo wa miaka mitatu umepewa jina la ‘Kupima kwa ajili ya kujifunza Afrika’(AFLA)  na utatekelezwa katika Wilaya ya Temeke.

Muktasari:

  • Akizindua ufunguzi  wa utafiti huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Mkurugenzi wa Mafunzo  ya Elimu ya Juu kutoka wizara hiyo, Profesa  Sylvia Temu alisema utafiti huo wa miaka mitatu umepewa jina la ‘Kupima kwa ajili ya kujifunza Afrika’(AFLA)  na utatekelezwa katika Wilaya ya Temeke.

Dar es Salaam.  Chuo Kikuu cha Aga Khan kupitia Taasisi yake ya Kuendeleza Elimu kwa nchi za Afrika Mashariki (IED-EA) wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford  cha Uingereza na Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini, wameanza  utafiti wa kupima maendeleo ya elimu  ya msingi katika ufundishaji nchini.

Akizindua ufunguzi  wa utafiti huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Mkurugenzi wa Mafunzo  ya Elimu ya Juu kutoka wizara hiyo, Profesa  Sylvia Temu alisema utafiti huo wa miaka mitatu umepewa jina la ‘Kupima kwa ajili ya kujifunza Afrika’(AFLA)  na utatekelezwa katika Wilaya ya Temeke.

“Kinacholengwa zaidi katika utafiti huu ni kuwawezesha watoto waweze kuwa na mchango katika mkakati mzima wa kujifunza, waweze kusema ni kitu gani hawakijui na kitu gani wanakijua na wapi kuna matatizo ili walimu waweze kutatua changamoto  kwa kuzifanyia kazi na kufanya wanafunzi waweze kufanya vizuri,” amesema Profesa Temu.

Amesema lengo la utafiti huo  ni kuangalia umuhimu wa kupima maendeleo ya elimu  kwa mwanafunzi wa shule za msingi na jinsi upimaji huo ukifanywa vizuri unavyoweza kusaidia wanafunzi kuelewa masomo yako na hivyo vizuri katika mitihani yao.

Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuendeleza Elimu kutoka  Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Joe Lugalla alisema wameamua kufanya utafiti huo baada ya kubaini kuwa  maendeleo ya wanafunzi katika shule nyingi hapa nchini  yamekuwa  sio mazuri.