Utafiti wabaini asilimia 30 ya wanawake hunyanyaswa kazini

Kaimu Balozi wa Marekani, Dk Inmi Patterson (wa pili kulia mbele) pamoja na akinamama wakifurahia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kongamano la Wanawake lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana.  Picha na Venance Nestory

Muktasari:

  • Utafiti huo umefanywa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).

Dar es Salaam. Wakati leo ikiwa ni Siku ya Wanawake Duniani, utafiti umebaini kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanawake nchini wanakumbana na ukatili wa kijinsia mahala pa kazi.

Utafiti huo umefanywa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).

Hata hivyo, kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani inasema: “Wakati ni huu: Wanaharakati wa vijijini na mijini wako tayari kubadili maisha ya wanawake.”

Kitaifa, kauli mbiu inasema: “Kuelekea uchumi wa viwanda: Tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake vijijini.”

Tucta wamefanya utafiti huo kwa kutumia sampuli za wafanyakazi wa hotelini na shambani na kubaini kuwa wanawake wanaofanya kazi katika mashamba wanaathirika zaidi.

Akizungumzia utafiti huo katika kongamano la wanawake lililofanyika jana jijini hapa na kujadili ukatili wa kijinsia katika maeneo ya kazi, naibu katibu mkuu wa Tucta, Jones Majura alisema ukatili wa kijinsia mahala pa kazi umerudi kwa kasi katika miaka ya karibuni.

“Sheria ya ajira namba sita, kifungu cha saba ya mwaka 2004 imemuagiza kila mwajiri aweze kujisajili kwa kamishna wa kazi na kuhakikisha anazingatia sera inayokataza ukatili wa kijinsia na unyanyasaji,” alisema Majura.

Pia, aliwataka wanawake kujitambua na wasikubali kutoa rushwa ya ngono.

Majura alisema sasa kuna tatizo la ajira, wasichana wengi wapo mtaani na wanapokwenda kwenye sekta mbalimbali kutafuta kazi wanalazimishwa kutoa rushwa ya ngono ili wapatiwe ajira.

Majura alitolea mfano akisema kuna wanawake wengine wanatambua kuwa wananyanyaswa lakini kwa kuwa ajira hawana wanaona ni bora wakubali kutoa rushwa ya ngono.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Tucta, Rehema Ludanga aliwataka wanawake wanaonyanyaswa wapeleke malalamiko yao na watayafanyia kazi ili kuhakikisha wanapata haki zao.

Alisema wanawake hunyanyaswa kijinsia kwa kuwa hawajui sheria, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha wanawake hao wanajitambua na kujua haki zao za msingi.

Kuhusu changamoto ya likizo ya uzazi Ludanga alisema likizo ya uzazi ipo kisheria lakini haizingatiwi.

Alisema mwanamke anapojifungua anatakiwa apewe likizo ya siku 84 lakini aghalabu waajiri hutafuta mwingine wa kujaza nafasi yake pindi anapokuwa likizo ya uzazi.

“Huo ni unyanyasaji wa kijinsia kisheria mama akiwa mzazi anatakiwa apewe likizo na siyo kumfukuza kazi, hivyo kama kuna anayekutana na unyanyasaji huo, aje haraka ili tuufanyie kazi, lengo ni kutokomeza vitendo hivyo,” alisema Ludanga.