Utashi wa kisiasa unavyoliingizia Taifa gharama

Muktasari:

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili wamesema hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo wananchi wataanza kuchagua chama badala ya mtu.

Dar es Salaam. Utashi wa kisiasa wa wabunge kuvihama vyama vyao umetajwa kulisababishia Taifa hasara kutokana na Serikali kutumia fedha nyingi kugharimia chaguzi za marudio.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili wamesema hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo wananchi wataanza kuchagua chama badala ya mtu.

Wamesema katika utaratibu huo, ikiwa mbunge atahamia chama kingine, chama chake cha awali kitapitisha mtu mwingine kuchukua nafasi yake, bila kulazimika kuingia kwenye uchaguzi.

Hivi karibuni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alieleza jinsi ofisi yake ilivyookoa Sh156 bilioni ambazo zingetumika iwapo Serikali ingeshindwa kesi na kurudia uchaguzi katika majimbo 52.

Hiyo inamaanisha kwamba kwa wastani, Sh3 bilioni hutumika kugharimia uchaguzi wa ubunge katika jimbo moja.

Hivi karibuni wabunge wawili wa upinzani, Dk Godwin Mollel wa Siha (Chadema) na Maulid Mtulia wa Kinondoni (CUF) walijivua uanachama wa vyama vyao na kujiunga CCM sawa na Lazaro Nyalandu ambaye alijiuzulu uanachama wa CCM na ubunge wa Singida Kaskazini na kuhamia Chadema.

Mbali na majimbo hayo ambako utafanyika uchaguzi unaotokana na utashi wa wanasiasa, majimbo ya Longido na Songea Mjini yatafanya uchaguzi kutokana na sababu zisizoepukika.

“Nadhani umefikia wakati wa wananchi kuchagua chama, mfano mbunge akihama chama chake, chama hicho kipitishe mtu mwingine kuwa mbunge wa jimbo husika bila NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kuitisha uchaguzi mwingine,” alisema Dk Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema.

Kwa kurejea wastani wa jimbo moja kugharimu Sh3 bilioni, majimbo hayo matatu yatatumia kiasi cha Sh9 bilioni. Gazeti hili limechambua kiasi hicho cha fedha na kubaini kuwa kinaweza kutumika kununua magari manne ya kubebea wagonjwa, kujenga zahanati tano, madarasa 400 na mashine mbili za CT-Scan kwa pamoja.

Magari moja la kubebea wagonjwa linagharimu Sh300 milioni, hivyo Sh1.2 bilioni za sehemu hiyo ya fedha zingeweza kutumika kununua magari manne na kuwezesha mikoa minne nchini kupata magari hayo.

Pia, zahanati moja yenye vifaa vyote muhimu, ujenzi wake unagharimu kati ya Sh600 milioni na Sh700 milioni. Hivyo, Sh3 bilioni zingeweza kutumika kujenga zahanati tano.

Pia fedha hizo zingeweza kujenga vyumba 400 vya madarasa kwa kutumia Sh3 bilioni. Ujenzi wa chumba kimoja cha darasa ni Sh7.5milioni.

Kipimo maarufu cha CT-Scan kinauzwa kwa wastani wa Sh900 milioni hivyo Sh1.8 bilioni zingeweza kutumika kununua mashine hizo mbili.

Wanasiasa, wasomi walonga

Katika ufafanuzi wake Dk Mashinji alisema, “Tukiwa na mfumo wa watu kuchagua chama tutaepuka gharama za chaguzi ndogo na hili wimbi la watu kuhama halitakuwa na athari zozote kwa maendeleo ya nchi. Unajua kinachoendelea sasa ni athari za demokrasia ambayo tumeichagua wenyewe.”

Alisema mgombea ubunge hubebwa na ajenda na ilani ya chama chake si yake binafsi, hivyo ikitokea akahama, chama alichokikimbia ndicho kinapaswa kuteua mtu mwingine kuwa mbunge, si uchaguzi kurudiwa.

“Huu utaratibu ndio unaotumika hata Afrika Kusini. Wananchi wanapaswa kuchagua chama si mtu.”

Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ngemela Lubinga alifafanua jambo hilo kwa kina na kusisitiza, “Kama wanataka kuondoa gharama ya uchaguzi wapeleke muswada bungeni maana suala la uchaguzi halipo kwa matakwa ya kikundi au matakwa binafsi, ni sheria na kanuni tulizojiwekea.”

“Kwamba ili tutekeleze demokrasia Tanzania yafuatayo yatatekelezwa, moja wapo ni ikiwa mbunge, diwani au mwenyekiti wa kijiji akifa au akijiuzulu lazima uchaguzi ufanyike.”

Alisema ikiwa wananchi watahoji jambo hilo na kupelekwa bungeni linaweza kubadilishwa na kwamba utaratibu huo ndio utekelezaji wa demokrasia.

Dk Charles Kitima wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) alisema jimbo likiwa wazi, uchaguzi unapaswa kufanyika ila kinachopaswa kujadiliwa ni baadhi ya wabunge kuwa kigeugeu na kujiuzulu ubunge na kujivua uanachama wakati waliomba kura wakiahidi kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema inasikitisha kuona gharama kubwa inatumika kurudia uchaguzi uliotokana na watu kujiuzulu wakati bado kukiwa na uhitaji wa dawa hospitalini, ajira kwa vijana, ujenzi wa barabara na shughuli nyingine nyingi za maendeleo.

“Kwa hiyo hili liwe fundisho kwa wananchi wakati wanapochagua wawatafakari wagombea, wasiwapigie kura vigeugeu,” alisema Dk Kitima.

Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Dk Jimson Sanga wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI). Alisema ni bora Serikali ingesitisha uchaguzi kwenye majimbo ambayo wabunge wake wanajiuzulu ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha ambazo zingetumika kwenye kazi nyingine za maendeleo ya wananchi.

Alisema haiingii akilini mbunge kujiuzulu kwa madai ya kuunga mkono sera na utendaji kazi mzuri wa Rais John Magufuli wakati uamuzi wake wa kuhama unapingana na sera ya kubana matumizi.

“Sasa kama wanaunga mkono kazi nzuri za Rais kwa nini wasipande majukwaani kuhubiri sera hizo badala ya kujiuzulu? Ni bora wangefukuzwa na vyama vyao kwa kuunga mkono jitihada za Rais jambo ambalo lingekuwa na namna nyingine ya kujadilika,” alisema Dk Sanga.

Alisema kazi ya mbunge kwenye jimbo ni kuwawakilisha wananchi na inapotokea Serikali inatekeleza sera za wananchi hao haimaanishi kuwa mbunge anatakiwa kuwasaliti na kuachia madaraka.

Aliongeza kuwa ipo miradi mingi ya maendeleo inayohitaji fedha nyingi ambazo badala ya kupelekwa huko, zitapaswa kutumika kwenye uchaguzi, hilo si jambo sahihi.

Katibu Mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi aliungana na Dk Mashinji na kusisitiza, “Iweje mbunge uhame kwa madai ya kuridhishwa na juhudi anazozifanya Rais Magufuli. Kwa nini juhudi hizo usiziige kwa kuliletea maendeleo jimbo lako.”

“Katika majimbo yao hakuna maji, umeme, huduma za afya ni duni lakini wanakimbia wananchi waliowachagua na kwenda kumuunga mkono Rais. Kwanini wasishirikiane na Rais kuwaletea wananchi maendeleo.”