Utata madai ya diwani ‘kumtwanga’ muuguzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule

Muktasari:

Kamanda wa polisi asema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kubaini ukweli ili hatua za kisheria zichukuliwe

Wakati jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma za diwani wa Bunambiyu Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga, Richard Sangisangi kumpiga makonde muuguzi wa Kituo cha Afya cha Bunambiyu, kiongozi huyo ameibuka na kukanusha madai hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga juzi, Sangisangi alisema tuhuma za yeye kumpiga na kumsababishia maumivu muuguzi Hilda Simon, zinasambazwa na wabaya wake kisiasa.

“Ni kweli Machi 8 nilifika kwenye kituo hicho cha afya baada ya kupokea simu ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kukosa huduma ya kuandikiwa rufaa ili mgonjwa wao ahamishiwe hospitali ya mkoa; lakini sikumpiga muuguzi zaidi ya kumsisitiza aandike rufaa kuokoa maisha ya mgonjwa,” alisema Sangisangi.

Akifafanua, diwani huyo alisema kulitokea mvutano kati yake na muuguzi huyo baada ya kukatalia ombi la kuandika rufaa akidai ndugu wa mgonjwa walikuwa wanamuingilia kwenye majukumu yake.

“Baada ya kuona anakaidi kuandika rufaa huku hali ya mgonjwa ikiendelea kuwa mbaya, nilimshika mkono kumwondoa kwenye kiti alichokalia ili kutoa fursa kwa muuguzi mwingine aliyekuwapo kuandika rufaa,” alifafanua,

Sangisangi alilazimika kuwasiliana na mganga mkuu wa wilaya ambaye alituma gari iliyomchukua mgonjwa huyo, Joseph Mbogo na kumkimbiza hospitali ya mkoa, ingawa alifariki dunia siku moja baadaye.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kubaini ukweli ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Ni kweli tumepokea tuhuma za diwani huyo (Sangisangi) kudaiwa kumpiga muuguzi, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Kamanda Haule.

Msajili wa Baraza la Uuguzi Tanzania, Lena Mfalila aliyetoa tamko kwa niaba ya Chama cha Wauguzi nchini alilaani tukio la muuguzi kupigwa na kiongozi huyo akiwa eneo lake la kazi.

Mfalila aliomba uchunguzi ufanyike ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa mtuhumiwa.