Utata wagubika wakazi kuzika jeneza bila maiti

Vijana wakiwa wamebeba jeneza tupu baada ya kulifukua kutokana na kuzikwa likiwa bila mwili wa marehemu Haruna Kyando (9) aliyekuwa mkazi wa Isanga jijini Mbeya. Picha na Godfrey Kahango

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea juzi baada ya mtoto huyo, aliyekuwa akiugua kifafa, kufariki Jumatatu na familia kuamua azikwe bila ya taratibu za kawaida za kuaga mwili ambazo hufanyika kwa kufunua kichwa cha marehemu na waombolezaji kupita kutoa salamu za mwisho.
  • “Sijui chochote kilichotokea hadi mwili wa mwanangu ukasahaulika ndani na kuzika jeneza tupu kwa kuwa sikuhusika kumuandaa marehemu na kumuweka kwenye jeneza,” alisema Jailo Kyando (36), ambaye ni baba wa marehemu.

Mbeya.  Tukio la wakazi wa Mtaa wa Kata ya Isanga jijini hapa kuzika jeneza baada ya kuacha chumbani maiti ya mtoto Haruna Kyando mwenye umri wa miaka tisa chumbani, limezua maswali kwa wakazi wa mjini hapa.

Tukio hilo lilitokea juzi baada ya mtoto huyo, aliyekuwa akiugua kifafa, kufariki Jumatatu na familia kuamua azikwe bila ya taratibu za kawaida za kuaga mwili ambazo hufanyika kwa kufunua kichwa cha marehemu na waombolezaji kupita kutoa salamu za mwisho.

“Sijui chochote kilichotokea hadi mwili wa mwanangu ukasahaulika ndani na kuzika jeneza tupu kwa kuwa sikuhusika kumuandaa marehemu na kumuweka kwenye jeneza,” alisema Jailo Kyando (36), ambaye ni baba wa marehemu.

“Sijui kilichotokea, lakini mwanangu alikuwa anasumbuliwa na kifafa kwa muda mrefu na leo (juzi) tulipoamka asubuhi tumekuta amefariki,” alisema Kyando.

Mkazi wa eneo hilo, Beny Chikwanda ambaye ni rafiki wa baba mzazi wa marehemu, alisema ilikuwa vigumu kwao kujua kama ndani ya jeneza kuna mwili wa marehemu kwa kuwa haukuagwa hadharani.

Alisema kilichofanyika ni kutoa jeneza ndani kisha kulibeba moja kwa moja kwenda makaburini. “Hili jambo  limetuacha na bumbuwazi. Tunajiuliza ilikuwaje wakati waombelezaji walikuwepo?” alihoji Chikwanda.

“Waombolezaji wamekuwa wakijiuliza maswali bila kupata majibu. Inakuwaje mtu aliyezikwa akaonekana ndani?”

Tukio hilo la aina yake lilisababisha kusambaa kwa taarifa nyingi tofauti zikiwamo zilizodai mtoto huyo amefufuka, huku wengine wakisema ni “maajabu ya mwisho wa dunia”.

Akisimulia kisa hicho, mwenyekiti wa mtaa huo, Fredy Mwaiswelo alisema mtoto Haruna alifariki Jumatatu asubuhi na kwamba  msiba uliendeshwa kwa taratibu za mazishi kufanyika.

Alisema saa 6:00 mchana, jeneza lilipelekwa msibani na kuwekwa chumbani  kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa kwenye blanketi na kulazwa juu ya godoro lililokuwa chini.

Alisema baadaye jeneza lilichukuliwa kupelekwa makaburini ambako lilizikwa.

Alisema baada ya waombolezaji kurudi nyumbani, waliambiwa na mmoja wao kuwa mwili wa marehemu huyo upo chumbani umelala eneo ulipokuwa awali.

Alisema taarifa hizo zilizua taharuki kwa waombolezaji na hivyo kulitaarifu Jeshi la Polisi ambalo askari wake walifika eneo hilo na kurejesha hali ya amani. Askari hao waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuihifadhi Hospitali ya Rufaa Mbeya.

“Mwili wa marehemu haukuagwa kama ilivyozoeleka kwa kuwekwa ndani na kila mtu kupita kutoa heshima zake. Badala yake, jeneza lilivyotoka ndani likabebwa moja kwa moja kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema baada ya kukamilisha mazishi, waombelezaji walirudi nyumbani kwa wazazi wa marehemu kwa ajili ya shughuli nyingine, lakini wakati wakiwa hapo ghafla mama mmoja ambaye hakumtaja jina, alitoka nje na kuwataka watu kutoendela kulia kwa kuwa mtoto aliyekuwa amekufa yupo ndani amelala kwenye godoro.

Alisema taarifa hiyo ilisababisha taharuki, huku wengi wakijiuliza maswali bila majibu. “Imekuaje mtu aliyetoka kuzikwa muda mfupi akaonekana ndani? Na watu waliohusika na kuuandaa mwili wa marehemu, hawakuona kwamba haujawekwa kwenye jeneza?” alisema akikariri maswali ya waombolezaji baada ya taarifa hizo.

Kadri muda ulivyokwenda ndivyo taarifa zilivyozidi kusambaa na hivyo kuvuta umati wa watu kutoka sehemu mbalimbali, baadhi wakienda makaburini kutaka jeneza lifukuliwe kuthibitisha kama mtoto huyo alifufuka.

Juhudi za kupata watu waliolitoa jeneza hilo chumbani na kulibeba kuelekea makaburini kujua kama walichukuliaje uzito wa jeneza hilo, hazikuweza kufanikiwa.

Jana, baadhi wa waumini wanaojulikana kama walokole wa Kanisa la Bonde la Baraka, walidai Haruna alifufuka kwa kuwa alikutwa akiwa hai ndani ya nyumba na polisi walimpeleka hospitali akiwa hai.

Lakini, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa, Thomas Isidory alisema polisi walipeleka mwili wa mtu aliyefariki muda mrefu uliopita.

“Nawahakikishia kwamba Haruna Kyando alifikishwa hapa akiwa mfu wa saa nyingi wala si kweli kwamba alikuwa hai,’’ alisema Isidory.

Polisi waingilia kati

Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa, Emmanuel Lukula alisema hadi jana ilikuwa haijafahamika  chanzo cha tukio hilo kama ni uzembe au tukio hilo lilifanywa na watu kwa malengo ya kupotosha ukweli.

Alisema taarifa za awali zinaonyesha kwamba mtoto alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa na kwamba alifariki kifo cha kawaida.

‘’Taarifa zilisema saa 6:00 mchana jeneza lililoletwa msibani na kuwekwa chumbani kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa kwenye blanketi na kulazwa chini kwenye godoro. Baada ya maombi yaliyoongozwa na waumini wa Bonde la Baraka,  vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa,’’ alisema.

Alisema polisi walilazimika kufika eneo hilo baada ya waombolezaji kurudi kutoka makaburini na walipoukuta mwili wa Haruna, kila mtu alikuwa akisema lake.

Alisema polisi kwa kushirikiana na wananchi waliamua kulilinda kaburi lisifukuliwe hadi jana saa 4:00 asubuhi  lilipofukuliwa chini  ya uangalizi wa polisi.

Baada ya kufukuliwa chini ya uangalizi wa polisi, viongozi wa serikali ya mtaa na ndugu, walikuta jeneza likiwa halina mwili ndani yake.

Baada ya kulichukua jeneza kaburini walilifungua na kukuta likiwa halina dalili kwamba liliwekwa mwili, akisema huenda waombolezaji walijichanganya  kabla ya kwenda makaburini.