Zati: Utawala wa kodi ufanyiwe marekebisho kuokoa mapato yanayopotea

Muktasari:

Wafanyabiashara visiwani humo wanaeleza juu ya kutokuwa na uhakika wa kiasi wanachotakiwa kulipa kutokana na kodi hizo kubadilika kila mwaka. Licha ya kubadilika, wanatakiwa kuzilipa kwenye mamlaka tofauti za umma hivyo kupoteza muda wa biashara.

Sekta ya Utalii ni muhimu kwa mapato ya mataifa mengi duniani, lakini changamoto inayoikabili ni kodi na tozo. Visiwani Zanzibar kuna takriban kodi na tozo 48 ambazo wajasiriamali wanatakiwa kuzilipa kutoka katika biashara wanazofanya.

Wafanyabiashara visiwani humo wanaeleza juu ya kutokuwa na uhakika wa kiasi wanachotakiwa kulipa kutokana na kodi hizo kubadilika kila mwaka. Licha ya kubadilika, wanatakiwa kuzilipa kwenye mamlaka tofauti za umma hivyo kupoteza muda wa biashara.

Wafanyabiashara hao hulalamika kutumia muda mwingi kutii masharti ya ulipaji kodi na tozo mbalimbali kuliko hata kufanya biashara yenyewe.

Kwa mujibu wa ripoti inayohusu Tathmini ya Kodi kwenye Sekta ya Utalii Zanzibar iliyoandaliwa kwa ufadhili wa taasisi inayoshughulikia uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara (BEST-Dialogue) ya mwaka jana, usumbufu huu unawagharimu walipakodi wa Zanzibar kiasi cha Sh7.14 bilioni kwa mwaka.

Kutokana na ukweli huo, Chama cha Wakekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati) kinasema gharama hizi zinatokana na kutumia muda mwingi na fedha kwa ajili ya kutafuta kuzitunza na taarifa sahihi.

Kujaza fomu za taasisi mbalimbali, kodi na tozo zenyewe, kutafuta ufafanuzi na ushauri wa kitaalamu pamoja na kuzielewa sheria mpya ni mambo yanayochangia gharama hizo.

Kutokana na ushauri ulitolewa na Dk Deogratius Mahangila na Wineaster Anderson waliofanya utafiti huo, Zati inatarajia kutoa msimamo wake na kuishauri Serikali namna sahihi ya kuratibu suala hilo kwa faida ya pande zote mbili.

Hali hii ya visiwani inasemakana kukaribiana na Tanzania Bara ambako nako kuna mlolongo wa kodi. Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na shirikisho la vyama vya utalii ilionyesha kwamba wafanyabiashara wa utalii hukumbana na kodi na ada kati ya 10 na 115 na tena zina mchakato na hatua ngumu kiasi cha kuchelewesha uwekezaji mpya katika utalii.

Hivi karibuni, Bunge lilipitisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ilianza kutekelezwa mwaka wa fedha wa 2016/17 Julai pamoja na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa sekta hiyo, Serikali haikubadili uamuzi.

Cha kufanya

Usumbufu utokanao na utawala wa kodi ni tishio la kuanzisha na kukuza biashara. Vilevile linafifisha ubunifu, kuongeza gharama za kufanya biashara na kupunguza ari ya wafanyabiashara kulipa kodi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejitajidi kurekebisha na kuimarisha sheria kadhaa za kodi, kuanzisha idara ya elimu kwa mlipakodi pamoja na kusogeza matawi ya benki karibu na ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi, Zati inapendekeza Serikali ikae na kuwashirikisha wadau juu ya namna sahihi ya kusimamia mapato yake bila kuwaathiri wafanyabiashara.

Kuimarisha ukusanyaji wa kodi na ada

Sekta hiyo inakadiria kuwa na kodi zipatazo 48 ambazo zinajumuisha kodi ya mapato, michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii, VAT na michango ya afya.

Inapendekezwa kodi hizi zingelipwa kwa mkupuo mmoja badala ya awamu tatu zilizopo ili kurahisisha utekelezaji wake na kuongeza mapato ya Serikali.

Sambamba na hilo, taarifa hii inapendekeza kuendelea kuunganisha kodi zinazowalenga walipa kodi wa aina moja, lakini kuwapo na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kuoanisha risiti zao.

Mfumo wa kielektroniki

Mfumo wa kielektroniki kwenye kodi unaelezwa kuwa muhimu ili kuongeza tija kwani utarahisisha ujazaji taarifa, kulipa na kusambaza stakabadhi kwa njia ya mtandao, hivyo kuondoa ucheleweshaji wa kuzunguka kwenye ofisi tofauti kwa ajili hiyo.

Licha ya kupunguza makosa ya kibinadamu katika kuingiza na kutunza kumbukumbu mfumo huu hutoa nafasi kwa maofisa wa kodi kuwasaidia wateja kutimiza wajibu wa kodi na kuongeza ufanisi.

Kwa mujibu wa Zati, hakuna malipo wala usajili wa kodi unaofanyika kwa njia ya kielektroniki visiwani Zanzibar. Zati inaishauri Serikali kugawa Mashine za Kielektroniki (EFDs) kwa wafanyabiashara na kuanzisha huduma kwa njia ya mtandao wa intaneti na simu za mkononi.

Mifano ya nchi zilizofanikiwa kwa hili zipo nyingi, ndani na nje ya Afrika. Rwanda imefanikiwa kupunguza muda wa kukamilisha mchakato wa kodi kutoka siku 23 hadi dakika chache baada ya kuanza kutumia mfumo huo.

Vituo vya pamoja

Kwa nia ya kupunguza muda unaotumika kukamilisha taratibu za kodi kwa wafanyabiashara kupeleka taarifa zao za mwaka TRA-Zanzibar, Bodi ya Mapato (ZRB), Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara (Brela) na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Zati inapendekeza kuwapo kituo kitachofanikisha suala hilo ndani ya muda mfupi.

Taasisi nyingine ambazo zinapaswa kupata taarifa za wafanyabiashara kila mwisho wa mwaka ni Wakala wa Kuchochea Uwekezaji Zanzibar (Zipa) na Tume ya Utalii Zanzibar (ZTC) bila kujali kuwa hazina mifumo thabiti ya kupeana taarifa ambayo ingeokoa muda wa kukamilisha mzunguko huo.

Kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kubadilishana taarifa, kila taasisi hupewa habari ile ile kwa muda tofauti hivyo Zati kupendekeza kuwapo kwa vituo vya pamoja (one-stop shop) ili kupunguza usumbufu na kuongeza ufanisi.

Uelewa wa sheria

Mafanikio ya ukusanyaji kodi yatapatikana endapo kila mlipaji atatimiza wajibu wake. Inaelezwa kwamba uelewa miongoni mwa wafanyabiashara juu ya wajibu huu ni mdogo, hivyo kuhitaji juhudi za makusudi kuongeza uelewa kwa wananchi.

Suala hili haliwaumizi wafanyabiashara pekee ila Serikali nayo inakosa mapato yake na kushindwa kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Zati inashauri Serikali kushauriana na wafanyabiashara yanapotokea mabadiliko katika sheria na kanuni za kodi ili kuondoa usumbufu na kupunguza malalamiko kwa ZRB.

Simu maalumu kwa wateja

Serikali ya Zanzibar imeanzisha idara maalumu kwa ajili ya elimu kwa mlipakodi. Hata hivyo, Zati inafikiri juhudi hizi zingesaidiwa na uwapo wa namba ya simu ambayo mteja atapiga bure kila anapokuwa na shida.

Kusimamia kodi

ZatiI inazishauri mamlaka zinazosimamia kodi Zanzibar zipime gharama za zinazotokana na utawala wa kodi ili kudhibiti hali hiyo na kuongeza makusanyo kutoka kwenye miradi halali iliyopo.

Ukurasa wa mazingira bora ya kufanya biashara umerudi kwenye gazeti la Mwananchi kila Alhamisi ukiwa na lengo la kuunga mkono jitihada za wajasiriamali nchini. Kwa maoni tuma ujumbe mfupi kwenda namba 0786240172 ukianza na neno RB kwa gharama za kawaida za ujumbe au baruapepe: [email protected]