Utekaji watu mashuhuri umegeuzwa ‘dili’ kwa magenge ya wahalifu

Muktasari:

Mara nyingi watu huhangaika kutafuta mali ili wawe matajiri na maarufu katika jamii huku wale wasio na mali hutembea wakiota ili siku moja wafikie ngazi ya ukwasi.

Dar es Salaam. Mara nyingi watu huhangaika kutafuta mali ili wawe matajiri na maarufu katika jamii huku wale wasio na mali hutembea wakiota ili siku moja wafikie ngazi ya ukwasi.

Hata hivyo, upande wa pili uliojaa ubaya wa kuwa tajiri na maarufu huwa hauzungumzwi kwa kina; upande huo ni matajiri kulengwa kuporwa au kutekwa na magenge ya wahalifu ili wadai fedha kama kuwakomboa.

Familia nyingi tajiri zimeathiriwa na matukio ya kuangukia katika mikono ya magenge au watu wanaotaka kujipatia utajiri wa haraka. Wakati mwingine watekaji huwaachia huru mateka wao, wawe watoto au wake wa mabilionea, lakini wakati mwingine hugeuka msiba kwa familia baada ya kushindwa kutekeleza matakwa ya watekaji.

Hapa chini ni orodha ya baadhi ya watoto au watu wazima matajiri duniani waliowahi kutekwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa familia tajiri kama inavyotokea kwa Mtanzania bilionea kijana Mohamed Dewji maarufu Mo.

 

Ivan Kaspersky.

Ikiwa jina hilo linaonekana maarufu basi uko sahihi maana huyo ni mtoto wa tajiri mtengenezaji wa programu za kompyuta, Eugene Kaspersky (mtengenezaji wa programu ya kupambana na virusi kwenye kompyuta iitwayo Kaspersky Anti-Virus).

Miaka saba iliyopita yaani mwaka 2011, genge la watekaji lililonuia kujipatia mamilioni kwa urahisi lilimteka Ivan mwenye umri wa miaka 20 na kumshikilia ili waweze kulipwa fedha za kumkomboa huko Moscow, Urusi.

Kutokana na makosa kadhaa waliyofanya watekaji, alipatikana akiwa mzima na salama na watekaji walikamatwa. Polisi waliweza kufuatilia nyendo zao kwa kufuatilia ishara ya simu ya mkononi ambayo waliiita Kaspersky Sr.

 

Bobby Greenlease

Ivan aliokolewa akiwa hai lakini Bobby Greenlease kijana mwenye umri wa miaka 6, mtoto wa milionea mfanyabiashara wa magari Robert Cosgrove Greenlease aliacha msiba mkubwa kwa familia yake.

Mnamo Septemba 28, 1953 watumiaji dawa za kulevya Carl Austin Hall na Bonnie Emily Brown Heady walipanga kumteka mtoto huyu asiye na hatia. Heady alijifanya kuwa shangazi wa mvulana huyo na akamshawishi mtawa katika shule ya Bobby amruhusu mapema, akisema familia ina jambo la dharura.

Kati yao Hall alisoma darasa moja na baba yake Bobby na alikuwa amepanga miaka mingi kuidhuru familia ya Greenlease. Hivyo, wawili hao walimchukua Bobby wakaenda naye hadi Kansas ambako walimpiga risasi kwa bastola akafa.

Baada ya mauaji, walitaka walipwe kikombozi cha dola 600,000. Familia ya Greenlease ikihaha kumuokoa mtoto wao hawakujua tayari alikuwa amekufa wakalipa. Haikuchukua muda mrefu kwa mamlaka kubaini ukweli na wawili hao walikamatwa, wakashtakiwa na wakanyongwa mwaka 1953.

 

Virginia Piper

Tukio jingine lililoshtua dunia lilikuwa la kutekwa mwaka 1972 kwa Virginia Piper mke wa Harry ‘Bobby’ Piper (Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uwekezaji ya Piper ya Minneapolis, Jaffray na Hopwood aliyechukuliwa wakati akihudumia bustani ya maua nje ya nyumba yake.

Badala ya kumweka kwenye chumba au nyumba mahali pengine, walimfunga kwenye mti kwa siku mbili mfululizo katika eneo la Jay Cooke Park karibu na Duluth. Watekaji walitaka dola 1,000,000 ili Virginia aachiwe salama, jambo ambalo mumewe alitekeleza. Baada ya watekaji kupokea fedha walimwachia. Watekaji hao hawakupatikana hadi 1977.

 

John Paul Getty

Pengine wakijaribu kujipatia mamilioni ya dola, baadhi ya watu huenda mbali zaidi na ndivyo ilimtokea John Paul Getty, mjukuu wa Jean Paul Getty, tajiri wa mafuta. Mwaka 1973 Getty akiwa na umri wa miaka 16 alitetwa kutoka Piazza Farnese huko Roma.

Watekaji walihitaji kikombozi cha dola 17 milioni, kiasi kilichoonekana kidogo tu kwa Jean Paul, siyo? Kwa bahati mbaya kwa kijana yule alikuwa anafahamika kwa tabia ya matata na aliwahi kufanya masihara ya kujiteka. Kutokana na hisia hizo, familia yake haikuchukulia kwa uzito suala la kulipa kikombozi.

Suala hilo lilipokuja kuonekana si mzaha baba yake John Paul alimwomba fedha Jean Paul lakini alikataliwa. Baada ya kukosa subira, watekaji walikata sikio la kijana na kulituma pamoja na kitita cha nywele kwenye gazeti na kuahidi kwamba watakuwa wanatuma kipande kimoja hadi kingine mpaka fidia itakapolipwa. Fidia ililipwa na Getty alirudi salama.

 

Patty Hearst

Pia tukio la kutekwa Patty Hearst mjukuu wa mmiliki wa kampuni ya uchapishaji William Randolph Hearst lilishtua pengine hiyo ni gharama za kuwa sehemu ya familia yenye hadhi ya juu sana.

Mwaka 1974, kijana huyo akiwa na umri wa miaka 19 alipigwa hadi kupoteza fahamu na akachukuliwa kutoka nyumbani kwao huko California. Genge lililojiita SLA kikundi chenye mrengo wa kushoto kilichokuwa kinaratibiwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha California kilimteka na kilitaka familia ya Hearst kutoa chakula cha thamani ya dola 70 kwa kila familia iliyopungukiwa huko California.

Gharama yake ingekuwa karibu dola 400,000,000. Baba yake Patty alichukua mkopo na akapanga kudondosha dola 2 milioni za chakula kwa jamii masikini ya eneo la Bay. Hata hivyo, kiasi hicho hakikuwaridhisha watekaji.

Ili kujiokoa binafsi, Patty alikubali kuwa mwanachama wa SLA, ambako alifanya kazi pamoja nao. Hatimaye alikamatwa na kuhukumiwa miaka 35 kwa wizi wa benki. Ni kama hadithi, sivyo?

 

Walter Kwok

Kisa kingine kilitokea mwaka 1990, Walter Kwok na ndugu zake wawili waliporithi mali ya baba yao tajiri mkubwa wa majengo Hong Kong, hali iliyomwezesha kuingia katika orodha ya matajiri katika jarida la Forbes.

Hiyo haikwenda bila kufahamika na wahalifu, kwani mwaka wa 1997 Kwok alinaswa na genge la wahalifu liitwalo ‘Big Spender’ aka Cheung Tze-keung. Mke wa Kwok, Wendy alizungumza nao na Kwok akaachiwa bila ushiriki wa polisi.

Ingawa haikujulikana rasmi ni kiasi gani kilicholipwa kutoka kwa Kwok au familia yake, Tze-keung baadaye alidai kwamba alikuwa amelipwa dola 600,000,000 ndipo Kwok aliachiwa. Baada ya Tze-keung kukamatwa kwa uhalifu mwingine, aliuawa katika Jamhuri ya Watu wa China Desemba 1998.

 

Teddy Wang

Tukio jingine la utekwaji lilimkumba Teddy Wang, mwenyekiti wa Chinachem na bilionea mmiliki wa majengo ya Hong Kong. Gazeti la Washington Post liliripoti kuwa katika miaka saba alitekwa mara mbili.

Hata hivyo, mara ya pili hakwenda nyumbani. Watekaji waliamini kuwa walipanga vizuri waweze kudai dola 60,000,000 ili aachiwe. Mke wa Wang alilipa nusu ya kiasi hicho na alitarajia kulipa nusu nyingine endapo mumewe angerejeshwa salama.

Polisi wa China walifanikiwa kufuatilia na Jeshi la Maji liliwafuatilia kwenye pwani ya Hong Kong. Watekaji walimtelekeza Wang baharini. Baadaye walikamatwa na sehemu ya fedha hizo zilirejeshwa.

 

Mfaransa

Halafu kuna mfanyabiashara wa Kifaransa ambaye hapendelei kutajwa jina lake lakini inajulikana alishikiliwa kwa miezi miwili huko Marbella. Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph, mfanyabiashara huyo alilazimishwa kukomba fedha zote kwenye akaunti zake za benki na kubadilisha utajiri huo kuwa miche ya dhahabu.

Watekaji walimwachia na walimtishia kumuua ikiwa asingewatumia Euro 100,000 kila wiki.