Utendaji wa wakuu wa mikoa, wilaya wakosolewa

Muktasari:

Imeelezwa Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1977, kifungu cha 15(1), inawapa wakuu wa mikoa na wilaya mamlaka ya kutoa amri ya kukamata na kumuweka ndani kwa saa 48 mtu yeyote iwapo mkuu huyo wa mkoa au wilaya ana sababu za kuamini kuwa mtu huyo anaweza kuvunja amani au kuvuruga utulivu.

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wamesema wakuu wa mikoa na wilaya wanatumia vibaya sheria kwa kuwaweka watu ndani.

Imeelezwa Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1977, kifungu cha 15(1), inawapa wakuu wa mikoa na wilaya mamlaka ya kutoa amri ya kukamata na kumuweka ndani kwa saa 48 mtu yeyote iwapo mkuu huyo wa mkoa au wilaya ana sababu za kuamini kuwa mtu huyo anaweza kuvunja amani au kuvuruga utulivu.

Hata hivyo, sheria hiyo inaweka angalizo kuwa viongozi hao wa mkoa na wilaya wanaweza kutumia mamlaka hayo iwapo wanaona uvunjaji huo wa amani na uvurugaji wa utulivu hauwezi kudhibitiwa isipokuwa kwa kumuweka mtuhumiwa ndani.

Baadhi ya waliohojiwa na Gazeti la Mwananchi walisema malengo ya sheria hiyo yalikuwa mazuri kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo na kusimamia masuala ya usalama lakini kwa sasa inatumiwa vibaya ‘kuwashughulikia’ watu wanaoonekana kuikosoa au kuipinga Serikali.