Uvuvi, ufugaji ulivyotishia kukimbiza wanafunzi shule wilayani Busega

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kabita wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu wakiwa darasani. Picha na Faustine Felician

Muktasari:

>>10%: Ufaulu wa matokeo ya wanafunzi wa shule za msingi katika Halmashauri ya Busega.

>> 523: Shule za msingi zilizopo katika Mkoa wa Simiyu zikiwamo za wilaya ya Busega.

>> 203,597: Wakazi wa Wilaya ya Busega kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2012

Busega.  Wanafunzi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za uvuvi, biashara ndogondogo na kuchunga mifugo ni moja ya sababu zinazochangia idadi kubwa ya wanafunzi wilayani Busega kuacha shule.

Wazazi pia wanatajwa kuwa miongoni mwa sababu za wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo, hivyo kuathiri maendeleo ya elimu. Takwimu zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2015 wanafunzi 131 walikatisha masomo kwa utoro sugu lakini idadi hiyo ilipungua mwaka 2016 ambapo kulikuwa na watoro 78 na mwaka 2017 walikuwa 32.

Jamii kutochangia elimu

Licha ya kuwa shule ni mali ya jamii, lakini kwa wakazi wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu kwa miaka mingi jamii imekuwa nyuma katika kujihusisha moja kwa moja na maendeleo ya shule ikiwamo kufuatilia maendeleo ya watoto wawapo shuleni.

Shule ya Msingi Mwamanyili imekuwa ikikabiliana na changamoto ya ushiriki hafifu wa wazazi katika masuala ya maendeleo.

Changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni utoro wa wanafunzi kwa wanaojiingiza katika shughuli za uvuvi pamoja na uchungaji wa mifugo na wengine uuzaji wa samaki, huku wazazi wengi wakiona ni mambo ya kawaida.

Ushuhuda wa mwanafunzi

Mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule hiyo, Sundi Stephano ana ndoto za kuwa mwalimu, lakini  zinaweza kuyeyuka kutokana na  mama yake kumzuia kwenda shule ili akauze dagaa.

Sundi anasema kwamba ugumu wa maisha kwenye familia yao unasababisha muda mwingine awe mtoro kwa kujihusisha na utafutaji wa chakula akiuza dagaa mitaani kutokana na shinikizo la mama.

“Baada ya wajumbe wa kamati ya shule ushirikiano wa walimu na wazazi kumfuata mzazi wangu walimwambia asiponipeleka shule watamkamata ndipo kesho yake nilipelekwa shule nikaanza maisha upya mpaka sasa naendelea vizuri kwenye masomo yangu,” anasema.

Mama wa mtoto huyo, Mary Mgema anasema kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo alishindwa kumpa mwanaye nafasi ya kwenda shule ili amsaidie kuuza dagaa.

Hata hivyo, ushirikiano wa wazazi na walimu umechangia kwa kiasi kikubwa mtoto huyo na wengine walioacha masomo katika shule hiyo iliyo umbali wa takribani mita 800 kutoka Ziwa Victoria waendelee na masomo.

Shule inasemaje?

Mwalimu Marsela Oweya wa shule hiyo anasema kwa sasa mtoto huyo anaendela vizuri baada ya kurejea shuleni.

“Toka tumpokee mwanafunzi huyu amekuwa akiendelea vizuri darasani licha ya changamoto ya utoro aliyokuwa nayo mwanzo na sisi walimu tunaendelea kumsaidia kwenye masomo yake ili aweze kuendana na wanafunzi wenzake na matokeo yake yamekuwa yakiridhisha kiwastani tofauti na mwanzo tulipompokea,” anasema Oweya.

Mwalimu huyo anasema ushirikiano wa wazazi na walimu umefanikisha kuwarejesha shuleni wanafunzi watoro zaidi ya sita wa darasa la sita ambao kwa sasa wanaendelea na masomo yao.

Mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika Shule ya Msingi Mwamanyili, Esther Paul anasema baada ya kugundua changamoto ya utoro kuwa kubwa waliweka mpango wa kuwabaini wazazi wa watoto watoro na kuzungumza nao.

Anasema baada ya kuzungumza nao waliwasukuma kuwarejesha shule watoto wao shule lengo likiwa ni kuwapa haki wanafunzi wote ya kupata elimu.

“Tuliwatafuta wazazi na kuongea nao na kuwataka kuwarejesha watoto wao ambao wanawatumia katika shughuli mbalimbali za kijamii zikiwamo kwenda kuchunga mifugo na kuuza mbogamboga, na tuliwapa muda wa kuwapeleka shuleni na wazazi wote wamekuwa wafuatiliaji wazuri wa watoto wao,” anasema.

Katika kuhakikisha maendeleo ya elimu yanafanikiwa zaidi katika kijiji hicho, mmoja  wa wajumbe wa UWW, Emmanuel Busweru alianzisha darasa la jioni nyumbani kwake, ambapo watoto badala ya kwenda kwenye vibanda vya sinema wanakutana hapo kujifunza.

Anasema alilazimika kuanzisha darasa hilo baada ya kuwaona wengi wao wanapoteza muda wa jioni kuzurura bila mpangilio kutokana na kukosa cha kufanya.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mwamanyili, Renatus Maige anasema shule hiyo ina wanafunzi 631 na walimu 11 na kwamba, utoro umepungua kutokana na ushirikiano wa wazazi na walimu ambao wamewakusanya watoro na kuwarejesha shuleni.

Maige anasema kwamba kutokana na ukaribu na Ziwa Victoria katika kijiji hicho, utoro uliwafanya baadhi ya wanafunzi kuwa wavuvi huku wakitumia mitumbwi katika kazi hiyo.

Anasema ili kuhakikisha wanahifadhi mazingira ya shule na kuwajengea uwezo wanafunzi kujiamini walianzisha klabu za mazingira kwa lengo la kuyahifadhi huku wakihakikisha wanafunzi wote wanashiriki.

Shule nyingine yaiga

Pamoja na Mwamanyili, shule nyingine iliyofanikiwa kupitia ushirikiano wa wazazi na walimu kufanya hivyo ni Shikizi iliyopo Kijiji cha Solima C, ambapo wazazi walichangia fedha na nguvu kazi kuijenga ili kuwanusuru watoto kutembea zaidi ya kilomita saba.

Kuanzishwa shule hii ni faraja kwa watoto wa Kijiji cha Solima C, akiwamo Esther Busweru na dada yake, Kamwa Robert ambao badala ya kutembea umbali huo kwa sasa wanatembea kilomita moja na nusu kufika shuleni.

Mwalimu wa kujitolea katika Shule ya Shikizi, Dotto Boniphace alichaguliwa na wananchi wa Solima C na kupatiwa mafunzo na shirika lisilo la kiserikali la Education Quality Improvement Programme (Equip) ili kufundisha wanafunzi wa darasa la utayari.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kabita, Judith Bubelwa anasema baada ya wazazi kubaini watoto wanashindwa kufika mapema shuleni kutokana na umbali wa walichangishana kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa darasa la awali.

Anasema kuwa wanafunzi wanaosoma darasa hilo la awali huwa wanaandikishwa kuanza darasa la kwanza katika shule mama ya Kabita licha ya changamoto kubwa ya mito na vichaka vyenye wanyama wakali.

Ofisa elimu anena

Ofisa elimu msingi wilayani humo, Gideon Bunto anasema kuna shule 86 na wanafunzi 72,634 ambapo wanaotarajiwa kuandikishwa mwaka huu kuanza darasa la kwanza ni 11,676.

Anasema licha ya changamoto mbalimbali utoro wa wanafunzi umetoweka baada ya shirika la Equip kutoa mafunzo kwa UWW namna ya kutokomeza tatizo hilo.

Bunto anasema kwamba katika kuboresha elimu, Equip iliwawezesha maofisa elimu kata vitendea kazi na usafiri wa pikipiki pamoja na kuwapatia semina ambazo zitawawezesha kusimamia elimu katika maeneo yao.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Anderson Njiginya anasema katika suala la elimu wilaya hiyo imepanda kutoka asilimia 50 mwaka 2016 hadi asilimia 60 mwaka 2017 na kimkoa imeshika nafasi ya tatu huku kitaifa ikishika nafasi ya 69.

Mkoa wa Simiyu una shule za msingi 523.