Uvuvi haramu washusha uzalishaji wa samaki

Muktasari:

Imeelezwa kuwa chanzo cha kushuka kwa uzalishaji huo ni uvuvi haramu unaoendelea ndani ya Ziwa Victoria.

Mwanza. Uzalishaji wa samaki katika Kiwanda cha Tanzania Fish Processors Limited (TFP) Igogo Mwanza, umeshuka kutoka tani 120 kwa siku hadi kufikia tani 25.

Imeelezwa kuwa chanzo cha kushuka kwa uzalishaji huo ni uvuvi haramu unaoendelea ndani ya Ziwa Victoria.

Akitoa taarifa ya uzalishaji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira waliotembelea kiwanda hicho, Meneja Rasimali Watu, Godfrey Samwel alisema licha ya uzalishaji kushuka kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 300 wa kudumu.

“Tunaamini Serikali itatumia njia bora za kukabiliana na tatizo hilo na muda siyo mrefu tatizo litakwisha,” alisema Samwel.

Alifafanua kuwa mapato ya kiwanda hicho kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilikuwa ni Dola 30 milioni za Marekani na walilipa kodi Dola 675,000 za Marekani.

Akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira, alisema wana mtambo wa kutibu majitaka unaotenganisha taka ngumu na maji na baadae taka hizo huuzwa kwa ajili ya chakula cha kuku.

Wajumbe wa kamati hiyo walipongeza jitihada za uzalishaji wanazozifanya na kukitaka kushirikiana kuwakamata wavuvi haramu ili kuongeza uzalishaji.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Kafumu alisikitishwa na upungufu wa uzalishaji ambao ni zaidi ya asilimia 80, hivyo alishauri Serikali kusimamia changamoto ya uvuvi haramu na utupaji taka ovyo ndani ya ziwa unaochangia kupungua kwa kina cha maji.

Pia, aliitaka Serikali kulinda vyanzo vya maji kuanzia vijito na mito inayoingiza maji ndani ya ziwa hilo.