Uwiano wa sera kuinua viwanda

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (kushoto), akihutubia kwenye mkutano mkuu wa Tano wa kitaifa wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Lilian Timbuka

Muktasari:

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa tano wa kitaifa waTaasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo, Philemon Luhanjo alisema ili sera ya viwanda ifanikiwe, kuna haja kwa Serikali kuhakikisha uwapo wa ustawi mkubwa kwenye sekta nyingine.

Dar es Salaam. Kuelekea uchumi wa viwanda hapa nchini, Serikali imeshauriwa kuwa na uwiano wa kisera kwa kuweka mkazo kwenye sekta nyingine kama kilimo, elimu na afya ili kurahisisha mabadiliko.

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa tano wa kitaifa waTaasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo, Philemon Luhanjo alisema ili sera ya viwanda ifanikiwe, kuna haja kwa Serikali kuhakikisha uwapo wa ustawi mkubwa kwenye sekta nyingine.

“Utekelezaji wa sera hizi za maendeleo ukienda kwa uwino utarahisisha mabadiliko kwa sababu haya mambo yana ingiliana na ili viwanda hivyo vifanye kazi vinahitaji malighafi, wataalamu wa kuvitunza na kuviendesha. Pia hawa wataalamu na wafanyakazi lazima wawe na afya ndiyo wataweza kutimiza wajibu wao vizuri,’’ alisema Luhanjo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuweka uwiano kwenye utekelezaji wa sera zake licha ya uwapo wa vipaumbele na ndiyo maana utekelezaji wa sera ya viwanda umekuwa na msisitizo kwenye sekta za afya, kilimo na elimu.

“Serikali inatambua kuwa ustawi wa viwanda unategemea sekta nyingine na kwasasa tunaweka jitihada kwenye masuala ya elimu, afya na tunawekeza kiasi cha kutosha bila kusahau kilimo na ufugaji,” alisema Dk Kijaji.

Akizungumzia mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu ‘Sera za kijamii katika muktadha wa mabadiliko ya kiuchumi Tanzania’ Dk Kijaji alisema, umefanyika wakati mwafaka huku akiahidi kutumia ripoti mbalimbali zilizowasilishwa kwenye mkutano huo kuandaa mipango ya kitaifa.

Awali, akizungumzia mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk Tausi Kida alisema unahusisha mijadala ya kina kutoka kwa washiriki wakiwamo wachumi, taasisi za kimaendeleo, wawakilishi kutoka sekta binafsi, taasisi za kiraia na ripoti za tafiti 11 zilitarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo.