Uzoefu usaidie kuimarisha ukanda huru wa biashara Afrika

Muktasari:

Makubaliano haya yalifanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe Machi 21 na ikaridhiwa shughuli za biashara huru zianze rasmi Oktoba na kuwanufaisha takriban watu bilioni 1.2 waliopo Afrika.

Mwezi uliopita, wakuu wa nchi 44 za Afrika kubaliana kuanzisha eneo huru la biashara. Eneo hili litakuwa kubwa kuliko maeneo yote huru kibiashara duniani.

Makubaliano haya yalifanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe Machi 21 na ikaridhiwa shughuli za biashara huru zianze rasmi Oktoba na kuwanufaisha takriban watu bilioni 1.2 waliopo Afrika.

Nchi 10 hazijayaridhia makubaliano haya kwa sababu mbalimbali ambayo ni lazima yapitishwe na mabunge ya nchi husika. Huenda nchi hizo zikajiunga baadaye.

Eneo huru

Nadharia za kiuchumi kwa ujumla na uchumi wa kimataifa kimahususi huunga mkono uwapo wa biashara huru kati ya nchi na nchi. Pamoja na mambo mengine, eneo huru la biashara huondoa vikwazo vya biashara kati ya nchi husika zilizokubaliana.

Vikwazo hivi ni pamoja na vya kodi na visivyo vya kodi kama vile ukomo wa kiasi cha bidhaa na huduma zinazoweza kuagizwa kutoka nchi moja. Bidhaa na huduma huuzwa na kununuliwa kwa uhuru bila vizuizi katika eneo hili.

Biashara huru imekuwa ikiungwa mkono kimataifa tangu zamani, miaka ya 1940 kulikuwa na makubaliano ya jumla ya biashara na forodha yaani General Agreement on Trade and Tariff (GATT). Makubaliano haya kwa sasa yanachukua sura ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) lililoanzishwa miaka ya 1990. Biashara huru ni afya na faida zaidi hasa kwa walaji kuliko biashara isiyo huru.

Kwenye baadhi ya maeneo dunini kuna biashara isiyo huru ambako nchi huwekeana vikwazo katika biashara za kimataifa. Huweza kuwa vikwazo vya kodi au visivyo vya kodi. Vikwazo vya kodi mfano ushuru wa forodha huongeza bei za bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi hivyo kupunguza ushindani ukilinganisha na bidhaa za ndani.

Njia hii hutumika kulinda wazalishaji wa ndani. Vikwazo visivyo vya kodi ni pamoja na ukomo wa bidhaa na huduma zinazoruhusiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Tabia za kulinda wazalishaji wa ndani kwa siku za karibuni imeongezeka hata kwa nchi za kibepari kama Marekani ambako falsafa ya uchumi wa soko huru imetamalaki kwa muda mrefu.

Wateja

Kimsingi, biashara huru ni habari njema kwa walaji. Inamaanisha uchaguzi mpana usio na ukomo wa bidhaa na huduma kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kwa sababu ya wingi wa bidhaa na ushindani, biashara huru humaanisha bei ndogo kwa walaji.

Hii ni neema kwa ustawi wao kiuchumi. Bidhaa zinapoingia bila ushuru wa forodha hupunguza bei. Zinapoingia bila ukomo wa kiasi huongeza wigo wa uchaguzi kwa mlaji.

Kwa walioishi Tanzania kabla ya zama za uchumi wa soko huru lililoruhusu bidhaa na huduma za aina mbalimbali kutoka duniani wataelewa jambo hili vizuri sana. Katika muktadha wa eneo huru la biashara Afrika, walaji watafaidi kutegemea na kiasi bidhaa na huduma wanachonunua kutoka nchi zilizo katika mpango huu.

Wazalishaji

Eneo huru la biasahara lina faida kadhaa kwa wazalishaji wa huduma na bidhaa kwa matumizi ya nchi husika. Pamoja na mambo mengine, eneo hili hupanua na kuongeza ukubwa wa soko kwa maana ya idadi ya wateja.

Hii ni kwa sababu hufungua mipaka. Badala ya kuwa na soko moja la ndani pekee. Kwa mfano, Tanzania sasa wazalishaji watakuwa na soko kubwa ndani ya nchi 44 zilizoridhia ushirikiano huo.

Hii itawawezesha kuzalisha na kuuza kwa wingi hivyo kupata faida kubwa. Soko huru huwezesha wazalishaji kuingia na kuzalisha ndani ya eneo la soko huru na kuuza popote ndani ya eneo hilo hivyo kupunguza bei ukilinganisha na kuzalisha nje ya soko.

Hata hivyo, eneo huongeza ushindani miongoni mwa wazalishaji. Wasio madhubuti huweza kuondolewa sokoni. Bidhaa kuingia bila ukomo na bila ushuru wa forodha hufanya wazalishaji wa ndani wapambane na wenzao kutoka nje.

Ni muhimu kwa nchi kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara ili wazalishaji wa ndani waweze kuhimili ushindani kutoka nje.

Mapato serikalini

Eneo huru la biashara huweza kupunguza mapato ya Serikali kutokana na kuondoa ushuru wa forodha. Mapato yatakayopungua yatategemea kaisi ambacho nchi husika inanunua kutoka ndani ya eneo huru na kiasi cha ushuru wa forodha kilichokuwa kikitozwa.

Kama nchi ilikuwa ikipata mapato mengi kutokana na ushuru wa forodha kwa bidhaa na huduma kutoka nchi wanachama wa umoja huo, basi itapoteza mapato haya. Itakuwa ni muhimu kutafuta mapato mbadala kuziba pengo hilo.

Maeneo mengine huru

Ni lazima ifahamike kuwa eneo la biashara huru Afrika halipo peke yake. Kuna maeneo mengine madogo kijiografia. Haya ni maeneo ya ushirikiano wa kikanda.

Maeneo hayo ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Maghabiri (Ecowas) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Maeneo haya yapo katika hatua mbalimbali za kuwa huru kibiashara. Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mfano, maendeleo ni makubwa na mtizamo ni kuwa na sarafu ya pamoja kisha shirikisho la kisiasa.

Wakati eneo huru la biashara Afrika linashangiliwa, ni muhimu pia kufikiria hatma na mchango wa maeneo haya madogo yaliyopo kwa muda mrefu. Pamoja na mambo mengine itakuwa muhimu kuyaimarisha maeneo haya madogo na kujifunza kutoka kwayo ili kuongeza uwezekano wa eneo huru Afrika kufanikiwa.