VIDEO: Bajeti Wizara ya Afya yapigwa panga

WAZIRI UMMY AJIFAGILIA BUNGENI ASEMA SEKTA YA AFYA IMEIMARIKA

Muktasari:

Bajeti hiyo inayoishia Juni mwaka huu ni Sh1.07trilioni.

Dodoma. Wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ikiomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh898.3bilioni kwa mwaka 2018/19, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii imesema bajeti hiyo ni pungufu kwa asilimia 19.6 ya ile ya mwaka 2017/18.

Bajeti hiyo inayoishia Juni mwaka huu ni Sh1.07trilioni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba alisema kupungua huko kutaleta athari kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kamati inahoji ni nini nia ya Serikali katika uimarishaji wa huduma za afya kwa wananachi?” alisema Serukamba wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake jana bungeni mjini Dodoma.

Alisema kwa mujibu wa makubaliano ya Azimio la Abuja la mwaka 2001 ambalo Tanzania ni kati ya nchi zilizosaini, Serikali ilipaswa kutenga Sh4.86 trilioni kwa bajeti ya afya sawa na asilimia 15 ya bajeti nzima kwa mwaka wa fedha 2018/19.

“Kamati inashauri Serikali kuongeza bajeti ya wizara hii kila mwaka ili kufikia asilimia 15 kama ilivyokubaliwa katika azimio,” alisema Serukamba.

Kamati hiyo pia ilibainisha jinsi sekta na vitengo vilivyo chini ya wizara hiyo vilivyopata fedha kidogo au kukosa kabisa katika bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo ilikuwa imetekelezwa kwa asilimia 57 hadi kufikia Februari.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipoulizwa sababu za kupungua kwa bajeti hiyo alisema atalitolea ufafanuzi suala hilo leo wakati akijibu hoja za wabunge watakaoijadili.

Fedha pungufu

Kamati hiyo ilisema kiasi cha fedha kilichotolewa katika bajeti ya wizara hiyo mwaka 2017/18 hakiridhishi na ni kinyume na matarajio ya mpango wa bajeti.

Serukamba alisema hadi kufikia Februari, wizara hiyo ilikuwa imepokea kiasi cha Sh576.5 bilioni sawa na asilimia 53 ya bajeti ya mwaka 2017/18 ya Sh1.07 trilioni iliyopitishwa na Bunge.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh190.75 bilioni zilipokewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara.

“Uchambuzi wa kamati umebaini kuwa katika matumizi mengineyo, wizara imepokea Sh59.3 bilioni sawa na asilimia 92.6 ya Sh64 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge. Fedha za miradi ya maendeleo, wizara ilitengewa Sh785 bilioni na hadi kufikia Februari Sh385.77 bilioni, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 49 kilipokewa na wizara ili kutekeleza miradi hiyo,” alisema Serukamba.

Alisema kati ya fedha hizo za maendeleo, Sh336.3 bilioni ni za kutoka vyanzo vya ndani na Sh449.5 bilioni kutoka vyanzo vya nje. “Kamati imebaini fedha zilizopokewa kutoka vyanzo vya ndani ni Sh64.7 bilioni sawa na asilimia 19 tu ya fedha zilizoidhinishwa. Fedha za nje zilizopokewa ni Sh321 bilioni sawa na asilimia 71.4,” alisema.

Alisema hadi kufikia Februari, wizara ilikuwa imepokea Sh15.46 bilioni sawa na asilimia 44 ya kiasi cha fedha kilichoidhinishwa cha Sh35.30 bilioni za matumizi ya kawaida katika Idara ya Maendeleo ya Jamii.

Kamati hiyo pia ilibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18 Taasisi ya Mifupa (Moi) iliidhinishiwa Sh3.8 bilioni kwa ajili ya kununua vifaa tiba, lakini fedha hizo hazijatolewa hadi sasa na kuishauri Serikali kuzitoa katika kipindi kilichobaki.

Serukamba alisema licha ya usambazaji wa dawa muhimu kuongezeka kwa asilimia 89.6, bado kuna changamoto ya dawa hizo kumfikia mgonjwa na kuitaka Serikali kuchunguza sababu za kuchelewa kwa dawa hizo.

“Serikali ifanye utafiti mdogo wa kuona dawa hizi zinaishia wapi licha ya usambazaji kuongezeka kwa asilimia kubwa ili kuitatua changamoto hiyo. Hitaji la mgonjwa mmoja mmoja ni kupata dawa pale anapohitaji kutibu ugonjwa unaomsumbua,” alisema.

Kamati hiyo pia imeishauri Serikali kutoa kiasi cha Sh10 bilioni za kununua dawa za kufubaza makali ya VVU mwaka 2017/18 kwa kuwa mpaka sasa hazijatolewa.

Waziri Ummy awasilisha

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Ummy alisema wizara imeendelea na maandalizi ya kuanzisha huduma za dharura katika barabara kuu ambayo inatekelezwa chini ya udhamini wa Benki ya Dunia (WB) ikihusisha ununuzi wa magari 12 ya kubebea wagonjwa, mabasi madogo mawili ya wagonjwa na magari matano ya uokoaji yenye uwezo wa kuinua magari yaliyopata ajali na kukata vyuma.

Alisema wizara imeandaa michoro ya vituo vya kutolea huduma katika barabara kuu vitakavyojengwa na kutumika kwa awamu ya kwanza inayohusisha barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Ruaha Mbuyuni.

Kuhusu ajira, alisema katika mwaka wa fedha wa 2017/18, wizara ilipata vibali vya ajira za watumishi 3,152 wa kada za afya.

Waziri huyo alisema wameajiriwa madaktari 45 wa daraja la pili, madaktari bingwa (24), madaktari washauri wawili, wauguzi daraja la pili (137) na kada nyingine za afya 3,081.

Hata hivyo, alisema watumishi wote walipatikana isipokuwa madaktari washauri.