VIDEO: Kamati Kuu Chadema yamuhoji Komu, Kubenea naye ndani

Muktasari:

Kikao cha Kamati Kuu ya chama kikuu cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania kimemaliza kumuhoji  mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu na sasa kinamuhoji mbunge mwingine wa chama hicho jimbo la Ubungo, Saed Kubenea.


Dar es Salaam. Kikao cha Kamati Kuu ya chama kikuu cha upinzani cha Chadema nchini  Tanzania kimemaliza kumuhoji mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu.

Baada ya Komu kumaliza kuhojiwa, mbunge mwingine wa chama hicho, Saed Kubenea (Ubungo) naye ameingia kuhojiwa.

Kikao hicho kinachofanyika katika ukumbi wa Ledger Plaza katika Hoteli ya Bahari Beach kinajadili masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama hicho likiwamo la wabunge hao.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hiyo kwa kile walichoeleza ni ya kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Komu ametoka katika kikao hicho saa 11:32 jioni  na alipotakiwa na MCL Digital kueleza nini alichohojiwa amesema hana mamlaka ya kuzungumzia chochote.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama changu sina mamlaka ya kuzungumza chochote  suala hilo lipo ndani ya kikao,” amesema Komu.

Wabunge hao leo saa 8:01 mchana walionekana nje ya ukumbi huo wakisubiri maelekezo ya kuingia katika kikao hicho.