VIDEO: Lady Jay Dee asema kulia sasa basi

JAY DEE ARUDI UPYA, ASEMA MACHOZI SASA BASI

Muktasari:

Mbali na wimbo pia Machi 31 anatarajia kufanya onyesho la ‘Anaweza Concert’, katika hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam. Malkia wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu Lady Jay Dee  amesema mwisho wake wa kulia ilikuwa 2004 na sasa ana matumaini makubwa, anasonga mbele.

Lady Jay Dee ameyasema hayo leo Machi 22, 2018  alipofanya ziara katika ofisi za  Gazeti la Mwanachi zilizopo Tabata Jijini Dar es Saalam, iliyoendana sambamba na kutambulisha wimbo wake mpya wa ‘Anaweza’ anaotarajia kuachia rasmi kesho.

Mbali na wimbo pia Machi 31 anatarajia kufanya onyesho la ‘Anaweza Concert’, katika hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo aliyewahi kutamba na vibao mbalimbali kikiwemo Usiusemee Moyo, Siku Hazigandi, Ndindindi, amesema katika albamu zake saba ambazo amezitoa hadi sasa alikuwa akiimba nyimbo za kuhuzunika na za machozi, lakini kuanzia mwaka 2004 kwake machozi hakuna tena na sasa ni matumaini.

Akizungumzia kuhusu wimbo wa Naweza, Lady Jay Dee amesema ni aina ya wimbo ambao umejaa matumaini ambapo mtu yeyote alikuwa amekata tamaa katika jambo akiusikiliza analiwazika.

Kuhusu onesho lake ambalo litakuwa ni mara ya pili kufanya ndani ya mwaka huu, Lady Jay Dee amesema atasindikizwa na wasanii mbalimbali akiwemo Nikk Mbishi, Alan Junior, Bushoke na Domo Kaya.

Albamu hizo ni Machozi (2000),  Binti (2003), Moto (2005),   Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013) na Woman (2017).