VIDEO: Masogange azikwa Mbeya, Makonda agharamia usafiri

Muktasari:

Mamia ya waombolezaji kutoka Dar es salaam na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya walijitokeza wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla.


Mbeya. Safari ya mwisho duniani ya aliyekuwa msaani maarufu aliyekuwa akipamba video za wanamuziki wa Bongo fleva, Agnes Gerald 'Masogange' imehitimishwa leo zaa tisa alasiri bada ya kuhifadhiwa kwenye nyumba ya milele nyumbani kwa wazazi wake Utengule – Mbalizi mkoani Mbeya.

Mamia ya waombolezaji kutoka Dar es salaam na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya walijitokeza wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla.

Akitoa salamu za rambirambi kutoka serikalini, Makalla amesema hakuna mtu anayejiandaa wala aliye tayari kwa ajili ya kifo, hivyo kifo cha Masongange ni kilelezo kwamba binadamu wote hapa duniani ni wasafiri.

‘Kifo cha Masogange kitukumbushe kwamba sote tutakufa, nimefurahi namna wasanii mlivyojipanga bila kujali bifu na tofauti zenu, katika hili mmekuwa pamoja,” amesema Makalla.

 

“Nilikuwa nafuatilia tangu msiba huu ulipotokea, mlikuwa pamoja na kwa mshikamano na sisi Serikali tunawapa pongezi sana.”

Makalla amewapongeza wananchi kwa namna walivyojitokeza kwa wingi na hiyo inaonyesha ndio utamaduni wa Mtanzania kushirikiana katika matatizo.

Akimshukuru Makalla kwa niaba ya wasanii wenzake, mwenyekiti wa wasanii hao, Steve Nyerere amesema, “hili ni pigo kwetu wasanii. Na sisi kama wasanii tumekubaliana kiasi tulichojichanga, kiasi fulani kitatumika kumlipia ada ya mwaka mmoja mtoto wa marehemu ambaye yupo darasa la saba lakini pia kumlipia bima ya afya endelevu.”

 “Tunakushukuru sana mheshimiwa mkuu wa mkoa...tunatambua thamani yenu kwetu wasanii kule Dar es Salaam tulikuwa na kiongozi wa kitaifa. Lakini leo tumekuwa na kiongozi wa Serikali wewe, mheshimiwa tunashukuru sana.”

Steve Nyerere amesema usafiri walioutumia kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya umegharamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda.