VIDEO: Mwananchi Communication yazindua Jukwaa la Fikra

Muktasari:

Mjadala huo utarushwa mubashara kupitia ITV/Radio One na mitandao ya kijamii ya MCL Digital

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) imezindua Jukwaa la Fikra litakalowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali na wananchi ili kujadili mada mbalimbali za kitaifa.

Mjadala wa kwanza utahusu magonjwa yasiyoambukiza ma unatarajiwa kufanyika kesho Juni 28, katika ukumbi wa Kisenga Hall kuanzia saa 3 kamili mpaka saa 5 usiku.

Mjadala huo utarushwa mubashara kupitia ITV/Radio One na mitandao ya kijamii ya MCL Digital. Katika mjadala huo, mada kuu ni; ‘Afya Yetu, Mtaji Wetu’ kuhusu.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo Juni 27, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi, Francis Nanai amesema mada mbalimbali zitajadiliwa za kitaifa, kizalendo kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa pamoja kuhusu baadhi ya matatizo na changamoto za nchi.

“Nina Furaha kubwa kuwakaribisha nyote kwenye mjadala  huu wa kwanza kabisa wa ‘MCL Jukwaa la Fikra’ tukiangalia magonjwa yasiyoambukiza. Tumeamua kuanza na mada ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu ya changamoto zinazotokana na ongezeko la magonjwa haya miongoni mwa Watanzania,” amesema Nanai.

 

Amesema jukwaa hilo linalenga kuwaleta pamoja viongozi wa Serikali, watunga sera, wadau mbalimbali, jumuiya ya kimataifa na kikanda, watendaji wakuu wa kampuni na mashirika mbalimbali nchini, wanadiplomasia, wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wasomi, wanafunzi, waathirika na Watanzania wote wanaoitakia mema nchi.

Nanai amesema lengo kuu ni kuendeleza mjadala wa jinsi ya kukabiliana na changamoto kadhaa zinazoikabili nchi hii na kuathiri mchango katika pato la taifa, kwani jukwaa hilo ni la kutafuta suluhisho la pamoja na si kunyoosheana vidole.

Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhaville ameishukuru MCL kwa ubunifu ambao alisema kuwa ni wa kisasa zaidi na utawapa wananchi na wadau uwanja mpana wa kujadili matatizo yanayowakabili na kupata suluhisho.