VIDEO: Polisi wamhoji Lema kuhusu sakata la kutekwa Mo

Muktasari:

  • Wakati mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiitikia wito wa polisi leo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Isaya Mungure amesema mbunge huyo anahojiwa kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji.

Arusha. Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Isaya Mungure  amesema mbunge wa chama hicho Arusha Mjini, Godbless Lema ameitwa polisi kufafanua kauli zake kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.

 

Leo Jumanne Oktoba 22, 2018 saa 4 asubuhi Lema ameripoti makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Arusha kama alivyotakiwa kufanya hivyo jana.

 

Akizungumza na MCL Digital, Mungure ambaye alikuwepo katika mahojiano ya awali kati ya Lema na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi amesema mbunge huyo ametakiwa kueleza ni kwa nini alitoa kauli kutaka wapelelezi wa nje ya nchi kuchunguza kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

 

“Amehojiwa juu ya kauli zake za masuala ya Mo na sasa anaendelea na mahojiano akiwa peke yake katika ofisi ya upelelezi,” amesema Mungure.

 

Mo alitekwa Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi na kupatikana Oktoba 20, 2018 baada ya watekaji kumtelekeza katika viwanja vya Gymkhana.