VIDEO: Shonza akataa utetezi wa Wema

Muktasari:

  • Mwigizaji Wema Sepetu anaendelea kuwa kwenye wakati mgumu hata baada ya kuomba radhi, huku utetezi wake ukionekana hauna mashiko.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amekataa kukubali utetezi wa mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu kwamba kosa alilofanya linatokana na utoto.

Shonza amesema Wema hana utoto wowote tatizo lake ameshindwa kujitambua kuwa yeye ni nani kwenye jamii.

“Wema hana utoto wowote, miaka 30 ukaseme mtoto, mie nina miaka 31 mbona sifanyi vitu kama hivyo na sijawahi kufanya,” amesema Shonza

Kufuatia hilo, amesema wizara kama mlezi wa wasanii itahakikisha inakemea vitendo hivyo na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wanaoitia doa tasnia ya sanaa.

“Bodi ya filamu imeshachukua hatua lakini bado mamlaka nyingine zitatekeleza majukumu yake katika hilo, asubiri adhabu ya (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ,” amesema.

Hilo linaungwa mkono na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mngereze ambaye amesema vitendo vichafu vya Wema vinajirudia mara kwa mara.

Msanii huyo juzi Alhamisi aliomba radhi kufuatia kusambaa kwa picha zake za faragha na Bodi ya Filamu Tanzania imemfungia kujihusisha na masuala ya filamu na uigizaji kwa muda usiojulikana.