VIDEO-Serikali kuvunja nyumba zilizojengwa bila kibali

Muktasari:

  • Waziri Lukuvi amesema atapambana na wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji watakaoshindwa kuwajibika.

Serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka alama za X na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali.

Pia, uwekaji alama na uvujaji utahusu majengo yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki za ardhi kwa dhuluma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hayo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Alikuwa ziarani kutatua mgogoro wa ardhi ambako ameagiza eneo lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa eka 12,750 lirejeshwe serikalini kwa kuwa utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa.

Taarifa iliyotolewa na wizara leo Jumapili Oktoba 22,2017 imeeleza waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela linaanza pale wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji wanapoacha majengo kuibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndiye anayejenga.

“Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza wakurugenzi, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka X katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa dhuluma,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema atapambana na viongozi hao pale atakapokuta majengo katika miji yasiyo na vibali vya ujenzi, yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika kiwanja cha mtu mwingine.

Amesema pia atapambana na viongozi wanaoshindwa kufuatilia kwa kuyavunja au kuyaweka alama ya X majengo hayo, kwa kuwa huo ni uzembe unaotokea nchi nzima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen ameahidi kufanyia kazi maagizo hayo kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa huo katika masuala yote ya ardhi.

Wakati huohuo, Lukuvi amesema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.

Amesema kuna changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi lakini fedha wanazitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, Dubai na kwingine duniani.

“Haiwezekani mtu atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo,” amesema.

Waziri Lukuvi amesema, “Kwa hiyo wizara imekusudia mwezi ujao kupeleka bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka 1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana,” amesema.

Amesema marekebisho haya yanalenga kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa zitumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo katika benki.

Waziri Lukuvi amesema tathmini iliyopo inaonyesha baada ya wawekezaji kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana, fedha hizo hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote nchini.

Amesema kuanzia Novemba, 2017 tatizo hilo litakwisha kwa kuwa jukumu hilo zitapewa benki na wakopeshaji watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika benki husika.

“Kama benki husika haitawafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, Serikali itamnyang’anya mkopeshwaji shamba hilo kwa kuwa atakuwa amekiuka sheria halafu benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleze shamba lile itakuwa imekula hasara,” amesema.

Mwisho.