Tuesday, September 11, 2018

VAT umeme wa Zanzibar watikisa Bunge Dodoma

Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba

Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi (kushoto) akizungumza jambo na Mbunge wa Welezo, Saada Salum Mkuya nje ya ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma jana. Picha na Filbert Rweyemamu 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Sakata la umeme unaokwenda Zanzibar kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat), jana lilitikisa Bunge kwa mara nyingine baada ya mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya kueleza wawakilishi wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) waliofika kujadili suala hilo walizuiwa nje ya jengo la Bunge.

Akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 3 wa mwaka 2018, Mkuya alisema alitegemea marekebisho hayo yangefuata ahadi ya Serikali ya kuleta marekebisho ya Sheria ama taarifa kuhusu sheria ya Vat.

Mkuya alinukuu maneno ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama yaliyopo katika taarifa rasmi ya Bunge (hansard) kuwa sheria zinatakiwa kufanyiwa kazi ili kuliweka jambo hilo sawa.

Aliendelea kusema kuwa Mhagama aliahidi watakapokutana katika mkutano huu wa 12, tatizo hilo litakuwa limemalizika na kuondoa wingu ambalo upande mmoja unaonekana kunyanyasika.

Alisema sio katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 2, namba 3 kunakoonyesha marekebisho wala taarifa juu ya kutekelezwa kwa ahadi hiyo.

Sakata hilo liliibuka Juni 28, wakati Bunge likipitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018/19 ambapo Mkuya aliyewahi kuwa waziri wa Fedha na Mipango alitaka Zanzibar kuondolewa suala la Vat katika umeme.

Baada ya hoja yake kutopatiwa ufumbuzi mbunge huyo alionekana akitoa machozi huku Spika Job Ndugai na Serikali wakiahidi kulifanyia kazi.

Jana, Mkuya alisema Serikali ya Zanzibar inabidi itoe Sh700 milioni kwa ajili ya malipo ya Vat na kwamba awali baada ya ahadi ya Serikali aliwaambia Wazanzibari kuwa watapata nafuu Septemba.

“Mheshimiwa Spika tuende wapi? Tuseme wapi? Hakuna hata taarifa ya kusema haya mambo yanaendelea. Mimi sikuwa na hoja naungana na Serikali kuhusu muswada lakini nimekuwa disappointed (nimefadhaika) kuona marekebisho ya sheria ya Vat ama maelezo yake hayamo kama mlivyoahidi,” alisema.

“Jambo dogo ambalo linakwaza na linasababisha maendeleo yazorote kwa upande mwingine wa Muungano (Zanzibar). You are doing very good job (Mnafanya vizuri sana) kwa upande wa United Republic of Tanzania (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).”

Hata hivyo, alisema kuna vikwazo kama hivyo ambavyo si vya lazima vinavyosababishwa wakwame. Alisema katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini aliitwa meneja wa Zeco na mtu mwingine kwa ajili ya kujadili deni la shirika hilo, lakini kwa bahati mbaya watendaji hao hawakupata ruhusa ya kuingia ndani ya jengo.

Hata hivyo, alihoji kwa nini hadi leo katika marekebisho ya sheria mbalimbali hakuna kifungu kinachohusu jambo hilo wakati ahadi ilitolewa tangu Juni 28 katika mkutano wa Bunge la Bajeti.

Nduga aagiza

Spika Ndugai alitaka wajumbe wa kamati hiyo kufafanua ni kwa nini waliwaita wawakilishi kutoka Zeco, lakini wakawazuia getini.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Zubeda Sakuru alikiri kuwa ni kweli walikuwa na mjadala wa deni la Zeco.

“Ni kweli tulikuwa na mjadala ambao ulikuwa unajadili deni la Zeco lakini ulishindikana kutokana na taratibu zinazosemekana ni chini ya ofisi yako, kwamba watu wa upande ule hawatakiwi kuongea na upande wa Muungano,” alisema na kuungwa mkoano na Ajali Akibar (Newala-CCM).

Baada ya maelezo hayo, Spika Ndugai alisema kamati hiyo ilikosea kutorudi kwake kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusiana na jambo hilo.

“Wakati mwingine watendaji wetu wanapenda kublock (kuzuia) vitu, yaani watu wanafikiri huku serikalini ukiwa unakwamisha jambo ni mtendaji mzuri,” alisema.

Aliahidi kulifuatilia kwa karibu jambo hilo na kuwataka wabunge linapotokea jambo lolote kuwasiliana naye. “Kwa sababu sote tunajenga nyumba moja si watu wanaotoka Egypt wala Sudan wote ni Watanzania. Hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Spika Ndugai aliendelea kusema, “haya makatibu tuambieni sasa mambo ya Zanzibar? Jibuni nyie sasa? Ni matatizo madogo madogo tu yupo mtu alifanya mambo ya ovyo sasa siwezi kujua kwa sasa hivi. Ni mapema mno nitafutilia baadaye, lakini nawaahidi jambo kama hili halitajirudia tena. Ni jambo la ovyo tu.”

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula alikiri kamati yake kukutana na Wizara ya Nishati, lakini wakati wanaandaa ratiba ilibainika kuwa ni vyema Zeco wakaalikwa na wizara.

Hata hivyo, alisema wakati wanafanya kikao walipata taarifa kutoka ofisi ya Bunge kuwa hakukuwa na kibali cha kamati yake kufanya mazungumzo na Zeco na kwamba, waendelee na nishati wakati utaratibu mwingine unaendelea.

“Tulifanya mazungumzo na wizara na wakatueleza maendeleo ya jambo hili. Kimsingi hatukuridhishwa na spidi,” alisema.

-->