Veta, Airtel watoa elimu ya ufundi kupitia simu

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Magilatech Company Ltd Godfrey Magila na mtaalamu wa teknolojia akitoa mafunzo kwa vijana waliodhuria semina kuhusu umuhimu wa kusoma kwa kutumia mtandao kupitia application ya VSOMO inayotumiwa na Veta kwa kushirikiana na Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel iliyofanyika makao makuu ya kampuni hiyo ya simu Morocco jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

  • VIjana 30,000 wapakua application ili kujisomea
  • Mwisho wa mafunzo hupata vyeti kama walio darasani

Dar es Salaam. Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikia na mamlaka ya elimu ya ufundi Stadi (Veta) leo Septemba 6 wametoa mafunzo kwa vijana mkoani Dar es Salaam itakayowawezesha kuongeza ujuzi na kuenda sambamba na mahitaji ya soka la ajira na kujiajiri.

Mafunzo hayo yenye lengo la kutoa fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia ushirika wa watoa huduma hao yanalenga kuwawezesha vijana nchini  kujiendeleza kielimu kupitia application ya VSOMO kwa kupata masomo ya ufundi stadi ya Veta kupitia simu zao za mkononi.

Akiongea wakati wa semina hiyo, Meneja Mradi wa Airtel, Jane Matinde, amesema wameamua kufanya hivyo ili kuongeza uelewa kwa vijana juu ya fursa za ajira zilizopo sokoni.

“Tunao wateja vijana zaidi ya 30,000 ambao wamepakua application ya VSOMO na kati yao 9,000 wamejiandikisha ili kusoma kwa mtandao lakini idadi ya waliopata vyeti bado ni wachache. Hivyo tumeona ni vyema kujikita katika kutoa elimu na kuwahamasisha watanzania kutumia teknolojia hizi za kisasa kujisomea wakati wowote mahali popote kupitia simu zao,” amesema.

Ametoa wito kwa watanzania, hususani vijana, kuchangamkia fursa hiyo kwa kupakua application ya VSOMO kwenye simu zao na kusoma kozi hizo za ufundi ambazo gharama yake ni Sh120,000.

Kwa upande wake mtaaalamu wa teknolojia na Mkurugenzi wa Magilatech Company Ltd Godfrey Magila, amesema tekonolojia inakuwa kwa kasi sana hivyo ni muhimu kuitumia kuleta tija katika biashara, kilimo, elimu na kadhalika.

Meneja Mradi wa VSOMO kutoka Veta, Charles Mapuli, amesema ushirikiano wao na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kumeongeza wigo katika kutoa elimu ya ufundi na kuwafikia watanzania wengi Zaidi.