Wanafunzi 35 wapata ujauzito Longido ndani ya miezi sita

Muktasari:

Wilaya ya Longido,Monduli na Arumeru zinaongeza kwa kesi za ukatili dhidi ya akinamama na watoto.


Arusha.Wanafunzi 35 wa shule ya msingi na sekondari wilayani Longido wamepewa mimba kati ya mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Longido,Atuganile  Chisunga, ametoa taarifa hiyo leo Juni 13  katika mkutano wa kujadili ukatili wa wanawake na watoto ulioandaliwa na mtandao wa mashirika ya wafugaji na wawindaji  wa asili (PINGOs Forums).

Chisunga amesema licha ya wanafunzi hao 35 kupata mimba,pia halmashauri hiyo imeokoa mabinti saba  walioolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 15.

"Kati ya watoto waliopata mimba, 27 walikuwa wanasoma shule za sekondari na wanane  ni wanafunzi wa shule za msingi" amesema.

Amesema katika wilaya hiyo pia bado ina changamoto ya watoto kukeketwa lakini pia unyanyaswaji wa wanawake ikiwemo kufanyiwa ukatili wa kingono,kiuchumi na kijamii.

"Bado wanawake wanachapwa viboko kati ya 40-70 ,bado wananyimwa haki kumiliki ardhi,wananyimwa haki nyingi za kijamii" amesema

Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria  wanawake,(TAWLA)Upendo Mutazi amesema,Wilaya ya Longido,Monduli na Arumeru zinaongeza kwa kesi za ukatili dhidi ya akinamama na watoto.