Vifaru vyarandaranda jijini Harare

Muktasari:

Aidha vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba msafara mkubwa wa wanajeshi wenye silaha ulizingira kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ZBC. Kadhalika Shirika la Reuters limesema vifaru vinne vilionekana mitaani.

Hali ya sintofahamu imejitokeza katika jiji la Harare baada ya vifaru kuonekana vikielekea mjini ambako vilitumika kufunga barabara kubwa za kuingia na kutoka nje.

Aidha vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba msafara mkubwa wa wanajeshi wenye silaha ulizingira kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ZBC. Kadhalika Shirika la Reuters limesema vifaru vinne vilionekana mitaani.

Baadhi ya watu walianza kusambaza picha za magari ya kijeshi kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi walisema (mapinduzi) lakini gazeti la Independent la Uingereza limeshindwa kuthibitisha ukweli wa picha hizo na msafara wa magari hayo ya kijeshi.

Hata hivyo, tukio hilo limekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi Jenerali Constantino Chiwenga kutishia kuingilia kati na akaagiza “kusitishwa” mara moja ufukuzaji wanachama kutoka chama cha Zanu PF cha Rais Robert Mugabe kufuatia kufutwa kazi kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.

Jenerali Chiwenga akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na walau makamanda 90 wa ngazi ya juu kwenye makao makuu ya jeshi, Jumatatu alisema: "Ufukuzaji huu unaolenga wanachama wa chama wenye uhusiano na harakati za ukombozi lazima ukome mara moja."

Ripoti zinasema kwamba jeshi limekuwa likimuunga mkono Mnangagwa kumrithi Mugabe, 93, lakini mke wa mzee huyo Grace ameibuka na kuwa mshindani mwenye nafasi kubwa.

Mnangagwa alifukuzwa serikalini na kwenye chama wiki iliyopita baada ya kushutumiwa kwamba alikuwa anapanga njama za kumwondoa mamlakani Mugabe. Mnangagwa amekimbilia uhamishoni.

Waziri wa Elimu ya Ufundi Jonathan Moyo amemkemea Jenerali Chiwenga lakini umoja wa vijana wa Zanu PF umesema “uko tayari kufa” ili kuitetea serikali ya Rais Robert Mugabe.

"Sisi kama vijana wa Zanu-PF ni simba aliyesimama imara na mwenye sauti, kwa hiyo hatutalemaa na kukunja mikono yetu wakati vitisho vikitolewa dhidi ya Mugabe," ilisema taarifa ya Katibu mkuu wa vijana wa  Zanu-PF Kudzai Chipanga.