Vifo vya uzazi vyapungua Kagera

Muktasari:

Vimepungua kutoka 73 mwaka 2017 mpaka kufikia 41 kwa takwimu za Januari hadi Juni.

Bukoba. Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua mkoani Kagera baada ya kuanzishwa kwa huduma ya uchangiaji damu salama kwa ajili ya huduma kamili za uzazi wa dharura.

Akizungumza na vyombo vya habari leo mkoani Kagera, Mganga Mkuu wa Mkoa wa huo, Dk Marko Mbata alisema tangu kuanza kwa mradi wa USaid ‘Boresha Afya’, vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua na hivyo kuonyesha matokeo chanya ya mradi huo.

Alisema vifo hivyo vimepungua kutoka 73 mwaka 2017 mpaka kufikia 41 kwa takwimu za Januari mpaka Juni.

"Kabla ya kuanza kwa huduma ya uchangiaji damu salama, takwimu za mwaka 2017 kulikuwa na vifo 73, kati ya hivyo 62 vilitokea katika ngazi ya vituo vya afya na 11 majumbani," alisema Dk Mbata.

Alisema vifo vingi vya akina mama vimekuwa vikisababishwa na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua kwa asilimia 25, maambukizi asilimia 15, kifafa cha mimba asilimia 30, kutoka mimba asilimia 15 na upungufu mkubwa wa damu mwilini asilimia 5 na sababu nyingine asilimia 15.

Dk Mbata alisema kwa sasa mkoa huo hauna shida ya damu kwani wameweza kutengeneza vituo vya kukusanya damu salama katika wilaya nne ikiwamo ya Misenyi, Bukoba Manispaa, Ngara na Biharamuro.

"Mkoa huu kwa sasa ni historia hatuna shida ya damu, tuna kituo hapa nje kinachotusaidia kukusanya damu na kwa kiasi kikubwa tunasaidiwa na mradi wa USaid Boresha Afya kwa kuwa tunapokwenda kukusanya damu lazima tuwe na mafuta, kuwalipa watumishi, vifaa kadhaa na viburudisho kwa wachangia damu, vyote wao wanatuwezesha, mkoa unasimamia,"

"Januari hadi Machi mwaka huu mkoa umekusanya jumla ya damu 4,050 na lengo la makusanyo ya mwaka ni chupa 21,380, kwa hiyo bado tunaendelea na makusanyo," alisema Dk Mbata.

Muuguzi Mshauri Hospitali ya Mkoa  Bukoba, Bashweka Amos alisema morali ya uchangiaji damu imeongezeka kwa walio wengi, hasa ndugu zao wanapoongezewa damu na wao huchangia.

"Hospitali ya mkoa hapa tunatumia uniti 5-15 kwa siku," alisema Amos.

Meneja Mradi wa USaid Boresha Afya mkoa wa Kagera, Fredrick Urembo alisema mradi huo unaohudumia halmashauri nane, unalenga kuboresha afya ya mama na mtoto.