Vigogo kortini wakidaiwa kuomba rushwa

Muktasari:

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali, Emmanuel Jacob amedai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya 2009 na 2012.

Dar es Salaam. Vigogo watatu wa  Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji,  Ephraim Mgawe (62) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya and Company Ltd, Kishor Shapriya (60) wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya Dola 4 milioni za Marekani (sawa na Sh8.9 bilioni)

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali, Emmanuel Jacob amedai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya 2009 na 2012.

Wakili Jacob alidai Mgawe, Bakari Kilo akiwa  Mkurugenzi wa Uhandisi TPA na Theophil Kimaro Meneja wa Ununuzi wa mamlaka hiyo kwa pamoja waliomba rushwa kupitia Kampuni  ya DB Shapriya ya kiasi hicho cha fedha  kwa Lengthton Offshore P+e Ltd  kama kishawishi ili kampuni hiyo ipate zabuni katika uwekezaji wa Single Point na Pipeline katika Ras  ya TPA Bandari ya  Mjimwema.