Vigogo saba Chadema waitwa polisi

Muktasari:

Akwilina, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

Dar es Salaam. Siku nne tangu kutokea kifo cha Akwilina Akwiline, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao Freeman Mbowe.

Akwilina, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

Mbali na Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wengine wanaopaswa kukamatwa ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu mkuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Pia wamo, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa akizungumza na Mwananchi jana jioni kuhusu wito uliopelekwa kwa viongozi hao alisema, “Hao ni watuhumiwa na kama wameitwa ni privilege (upendeleo/fadhila) tu, ila kwa yaliyotokea wanapaswa kukamatwa.”

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba juzi alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kufanya uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi Akwilina haraka na uwekwe wazi.

Kauli ya Kamanda Mambosasa ilitanguliwa na taarifa ya mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema aliyesema walipokea wito wa Jeshi la Polisi jana saa 10:51 jioni ukiwataka viongozi hao kuripoti jana hiyohiyo saa 11:00 jioni.

“Barua hiyo ya wito imeelekezwa kwa mwanasheria ambaye si mtendaji mkuu wa chama na pia imetolewa kwa viongozi niliowataja kana kwamba viongozi hao wapo pamoja muda wote jambo ambalo si sahihi,” alisema Mrema.

Alisema viongozi hao wametawanyika maeneo mbalimbali ya nchi katikakutekeleza majukumu yao, hivyo ni vyema Jeshi la Polisi likayaelewa mazingira hayo wakati wakiendelea na utaratibu wa kutekeleza wito huo na kuepuka kuwa sehemu ya propaganda za kisiasa zinazoendelea.

Mrema alisema walikuwa wanawasiliana na wanasheria ili kujua ratiba zao na za viongozi wanaotakiwa kuripoti polisi ili wapange jinsi ya kuutekeleza wito huo.

“Tunapenda kuwajulisha wanachama wetu na umma kuwa viongozi wetu wapo imara na wanaendelea kuimarika zaidi,” alisema Mrema.