Vigogo wanavyopigana vikumbo majimboni

Muktasari:

  • Huu ni wakati ambao shughuli za kijamii hufanywa kwa wingi na watu ambao wana mkakati wa kugombea uongozi katika maeneo fulani. Na hata wale ambao hawana nia hiyo, shughuli za kijamii wanazohusika hutafsiriwa kuwa ni kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu ujao.

Dar/mikoani. Unapobakia mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu, huhitaji darubini kujua kuwa kuna harakati au kuna vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni harakati kabla ya tukio hilo kubwa.

Huu ni wakati ambao shughuli za kijamii hufanywa kwa wingi na watu ambao wana mkakati wa kugombea uongozi katika maeneo fulani. Na hata wale ambao hawana nia hiyo, shughuli za kijamii wanazohusika hutafsiriwa kuwa ni kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu ujao.

Ni utekelezaji wa ahadi ambazo hazikuwahi kutolewa, hasa kwa wale ambao wanataka kupata uongozi wa kuchaguliwa kwa mara ya kwanza.

Kutoa misaada kwa vikundi, shughuli za michezo, kuchangia ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii kama hospitali, shule, visima vya maji, masoko, makanisa ni baadhi ya shughuli ambazo hutumiwa au ushiriki wake hutafsiriwa kuwa ni kujipanga kwa uchaguzi ujao.

Ingawa vitendo hivyo hivyo havitakiwi kuhusishwa na uchaguzi, kwa mujibu wa sheria, hali ndivyo ilivyo katika sehemu nyingi ambazo Mwananchi imefanya uchunguzi.

Katika maeneo hayo, vigogo, wakiwamo mawaziri ambao hawana majimbo, wabunge wa kuteuliwa na wakuu wa mikoa ndio wanaoonekana kupigana vikumbo katika majimbo ambayo baadhi yanashikiliwa na upinzani ingawa wamekana kuhusisha na kampeni za 2020.

Wakati vigogo hao wakikataa kuhusisha shughuli wanazofanya na kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo, wabunge wa majimbo hayo wamedai kushuhudia harakati hizo za wanaoweza kuwa wapinzani wao mwaka 2020.

Mikopo kwa wanawake 600 Arusha

Hali hiyo imeonekana mkoani Arusha ambako mkuu wake, Mrisho Gambo amekuwa akitajwa kulinyemelea Jimbo la Arusha Mjini, akihusishwa na shughuli za kijamii ambazo amekuwa akizifanya.

Katika siku za karibuni, Gambo aliwapa mikopo wanawake 600 wa jiji hilo kabla ya awali kusaidia kutolewa kwa mikopo ya pikipiki kwa vijana zaidi ya 100.

Shughuli nyingine ambayo ameifanya ni kuwezesha ujenzi wa kituo kikubwa cha afya katika Kata ya Murieti sehemu ambayo anaishi.

Hata hivyo, mara kwa mara Gambo, ambaye amekuwa katika uhusiano mbaya na mbunge wa sasa, Godbless Lema, amekuwa akikanusha kutaka kugombea jimbo hilo. Akizungumza katika kikao na viongozi wapya ya jumuiya ya wanawake ya Wilaya ya Arusha hivi Karibuni, Gambo aliwataka wana CCM ambao wanataka kugombea jimbo hilo kujitokeza sasa na kufanya kazi za kukiimarisha chama hicho huku akiahidi kuwa kwa gharama zozote mwaka 2020  jimbo hilo litarudi CCM.

Lakini, Lema alisema kwa sasa hawazi masuala ya uchaguzi na badala yake anatia mkazo katika masuala ya nchi pamoja na maisha ya wajukuu wake.

Lema alisema hashangazwi na kauli hiyo ya Gambo na kinachoendelea kwenye jimbo lake kwa kuwa anaamini kuwa ushindi wa uchaguzi siku hizi unategemea wasimamizi na sio wapigakura kama ilivyokuwa awali.

Mbeya Mjini na Rungwe Magharibi

Hali kama hiyo imejitokeza katika majimbo ya Rungwe na Mbeya Mjini ambako Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson anahusishwa na mipango ya kugombea ubunge kutokana na shughuli anazofanya.

Lakini suala lake lina utata kwa kuwa bado haijafahamika hasa anataka jimbo gani; Rungwe Magharibi ambako mbunge wa sasa ni Saul H. Amon (CCM), au Mbeya Mjini kwa Joseph Mbilinyi (Chadema).

Awali, naibu spika huyo alijikita kufanya shughuli za maendeleo wilayani Rungwe na kuhusishwa na harakati za kuwania Jimbo la Rungwe Magharibi, lakini kwa sasa upepo umegeuka kutokana na kuonekana zaidi mjini Mbeya, ambako huendesha mbio za marathoni kila mwaka kwa kutumia taasisi yake ya Tulia Trust.

Lakini, baadhi ya fedha zinazopatikana katika mbio hizo, pia hutumika kuchangia shughuli za kijamii wilayani Rungwe, ambako aliwahi kujihusisha na tamasha la nyimbo za injili. Taasisi hiyo pia ilijihusisha na utoaji mikopo kwa wajasiriamali wadogo.

Hoja za wanaomuhusisha na ubunge wa Mbeya Mjini zinatiwa nguvu na kitendo cha taasisi yake kufungua ofisi jijini Mbeya.

Mkoa wa Mbeya una majimbo saba ya uchaguzi na kati yake, majimbo sita na halmashauri zake zinaongozwa na CCM na jimbo moja pekee linashikiliwa na Chadema kwa vipindi viwili mfululizo.

Hata hivyo, Uchaguzi Mkuu uliopita ulikuwa na upinzani mkali katika majimbo ya Kyela na Rungwe Magharibi, ambako polisi walilazimika kutumia nguvu kutawanya wananchi kabla ya matokeo kutangazwa.

Kwa miaka mitatu sasa, Dk Tulia, kwa kutumia taasisi yake, amekuwa akiandaa mashindano ya riadha yajulikanayo kwa jina la Tulia Marathon ambayo huhusisha utafutaji fedha kwa njia ya udhamini ili kuiwezesha Tulia Trust kupata fedha za kusaidia jamii.

Dk Tulia pia amekuwa mstari wa mbele kushiriki katika shughuli za kijamii kama kutoa Sh10 milioni kwa waathirika wa moto ulioteketeza Soko la Sido lililopo eneo la Mwanjelwa Jijini Mbeya.

Dk Tulia alijitolea kukarabati chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Ruanda pamoja na kujenga vyoo katika shule ya Msingi Mapambano iliyopo kata ya Iyela jijini Mbeya.

Vilevile alitumia kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kufuturisha waumini wa dini ya Kiislamu, shughuli ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa dini pamoja na madhehebu mengine, wanasiasa, viongozi wa kimila na Serikali kutoka pande zote mkoani humo.

Hivi karibuni naibu huyo spika wa Bunge ametoa msaada wa vyakula wenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni kwa wajane na yatima wa dini ya Kiislamu kwa ajili ya sikukuu ya Eid el Fitr huku akiwaalika madiwani  wote wa Jiji la Mbeya na baadhi ya viongozi waandamizi wa umma kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kwenda bungeni.

Hata hivyo, Dk Tulia, ambaye kwa sasa ni mbunge wa kuteuliwa, alisema ni mapema kusema kwamba atagombea jimbo gani lakini wakati ukitafika atafanya hivyo bila kificho.

“Da hapa umeniotea,” alisema. “Lakini kwa kweli muda bado kuzungumzia jambo hilo, ila vuta subira nitasema kama nagombea na ni jimbo gani nitakwenda.”

Kwa upande wake, Sugu alisema anaamini mtaji wake ni wananchi na si fedha, akidai makada wa CCM ndio wanaotumia fedha na kueleza kuwa wapigakura hawatafanya makosa. “Nilishasema, sijawahi kukosa usingizi kuhusu CCM wanavyohaha hapa mjini. Mtaji wangu wa siasa ni watu na sio fedha,” alisema Sugu ambaye anaongoza jimbo hilo kwa kipindi cha pili mfululizo.

“Hao wanaotoka Dar wanakuja na fedha, (lakini) wataijua Mbeya wakati ikatapofika hiyo 2020.  Sina hofu kwa kuwa mimi na chama changu bado tuko vizuri.”

Jimbo la Iringa Mjini

Katika Jimbo la Iringa Mjini, ambako Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) anaongoza kwa kipindi cha pili mfululizo, nako kuna moto unawaka.

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Agustino Mahiga ndiye anayehusishwa na harakati za kulirudisha jimbo hilo CCM kutokana na kuonekana mara kadhaa katika shughuli za kijamii.

Mwezi Machi, Dk Mahiga kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la WorldShare la Korea Kusini, walianza ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kidamali, ujenzi ambao utagharimu Sh200 milioni.

Mei mwaka huu, Dk Mahiga alitembelea ofisi za timu ya Lipuli na kutoa msaada, lakini pia alishiriki futari na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani hapo.

Akizungumzia matukio hayo, Mchungaji Msigwa alisema hana shaka na wanaopita jimboni humo kwa kuwa yuko imara na kwamba ushindi kwake hauepukiki.

“Hakuna awamu ambayo nilishinda bila wao kuweka mtu,” alisema. “Najua CCM wamejipanga, lakini hata katika chama changu wako wanaotaka kugombea. Nasema labla wanipore kwa nguvu, vinginevyo nitashinda kwa kura nyingi.”

Jimbo la Tanga

Jijini Tanga, mzigo wa kulirejesha jimbo CCM unahusishwa na harakati za waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ambaye ameshiriki shughuli tofauti za kijamii, hasa kuisaidia klabu kubwa na kongwe ya Coastal Union hadi kuiwezesha kurudi Ligi Kuu Bara.

Mbunge huyo wa viti maalumu atakuwa na kazi ya kupambana na Mussa Mbarouk wa CUF iwapo ataingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Ummy pia aliisaidia klabu hiyo kumiliki eneo lililopo Kata ya Maweni jijini Tanga ili kujenga uwanja wa klabu hiyo na kuuomba ubalozi wa Uturuki msaada wa vyakula vya sikukuu ya Idd.

Waziri Ummy, anatajwa kuwa amekuwa akishirikiana na viongozi wa Coastal Union kutafuta fedha kwa ajili ya mishahara na gharama nyingine za klabu hiyo na amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha mashabiki wakati wa mechi muhimu za Ligi Daraja la Kwanza.

Hata hivyo, Juni 12, mbele ya viongozi wa CCM wa mkoa na wilaya, Waziri Ummy alikanusha uvumi kuwa anawania ubunge wa jimbo hilo. “Wakati wa uchaguzi bado. Kwa sasa tunafanya kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema.

“Ninachokifanya hapa ndicho ninachokifanya katika majimbo ya mikoa mingine. Siwezi kuacha kuwasaidia wana-Tanga wenzangu kwa sababu eti watasema nawania ubunge.”

Maneno hayo yaliungwa mkono na Mbunge wa Jimbo la Tanga CUF, Mussa Mbarouk alipozungumza wakati wa kukabidhi uwanja kwa klabu ya Coastal Union kwamba kuipandisha daraja Coastal Union ilikuwa ni mikakati iliyowekwa kwa pamoja na kwamba sasa viongozi hawazungumzii vyama wala kuwania ubunge bali ni Tanga kwanza.

Kasulu, Mayovu na Kigoma Mjini

Kwingineko, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako anahusishwa na mikakati ya kuwania moja kati ya majimbo wilayani Kigoma na Kasulu kutokana na misaada yake ya kielimu.

Miradi iliyopewa kipaumbele na waziri huyo ni ujenzi wa madarasa na ofisi katika Shule ya Msingi ya Uhuru na Karuta zilizopo mjini Kigoma, ukarabati wa Sekondari ya Kigoma lakini pia Shule ya Msingi Mwenge iliyopo mjini Kasulu.

Profesa Ndalichako aliyesoma elimu yake ya msingi shule za Mwenge iliyopo Kasulu na Karuta ya mjini Kigoma amekuwa pia akishiriki katika harambee za kuchangia shughuli za jamii kwenye taasisi za dini na uzinduzi wa albamu mbalimbali za kwaya.

Mkazi wa Mwanga mjini Kigoma, Maulidi Jumanne alisema safari za Ndalichako, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa, wilayani humo zinatafsiriwa kama njia mojawapo ya kujipanga kisiasa na kuandaa wafuasi kwa ajili ya kushiriki kura za maoni ndani ya chama chake.

Jimbo la Kigoma Mjini linaongozwa na Zitto Kabwe (ACT) na Kasulu Mjini likiwa chini ya Daniel Nsanzugwanko (CCM).

Katika harakati hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hajasalimika. Mbunge huyo wa kuteuliwa anahusishwa na Jimbo la Manyovu ambalo kwa sasa linaongozwa na Obama.

Hata hivyo, tofauti na Profesa Ndalichako, Dk Mpango anadaiwa kuendesha harakati zake za kisiasa kimya kimya huku akisaidiwa na baadhi ya wanachama wa CCM.

Katika moja ya hotuba zake mkoani Kigoma, Rais Magufuli aliwahi kunukuliwa akimsifia Dk Mpango kwamba ni kiongozi anayestahili kuwa mbunge wa eneo hilo.

Imeandikwa na Burhan Yakub, Godfrey Kahango, Mussa Juma, Antony Kayanda, Berdina Majige, Habel Chidawali na Tausi Mbowe.