Vijana waonywa kukimbilia mjini

Muktasari:

Rai hiyo ilitolewa juzi na Diwani wa Parakuyo ambaye ni mfugaji wa jamii ya Kimasai, Ibrahimu Oloishuro wakati akizungumza na wawakilishi wa vijana wa kabila hilo kupitia mashirika yanayoshughulikia wafugaji nchini.

Morogoro. Vijana wametakiwa kuacha tabia ya kukimbilia mijini kutafuta kazi za ulinzi na kuuza dawa za kienyeji badala yake wawasaidie wazazi wao kutunza mifugo.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Diwani wa Parakuyo ambaye ni mfugaji wa jamii ya Kimasai, Ibrahimu Oloishuro wakati akizungumza na wawakilishi wa vijana wa kabila hilo kupitia mashirika yanayoshughulikia wafugaji nchini.

Alisema kutokana na vijana kukimbia, wazazi huwatumia watoto kuchunga mifugo hali inayosababisha kuingia kwenye mashamba na kuzua migogoro ya wakulima na wafugaji.

Aliwataka wafugaji kwenda na wakati na kuacha ufugaji wa kuchunga porini badala yake waboreshe mazingira na wafuge kisasa.

Kiongozi mkuu wa jamii hiyo mkoani Morogoro, Laigwenani Lopejo aliitaka jamii hiyo kudumisha amani na upendo kwa wakulima.

Lopejo alisema mapigano hayawezi kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji bali mazungumzo.

Baadhi ya vijana walisema wanakimbilia mijini kutokana na hali ngumu ya maisha na ukosefu wa miundombinu katika maeneo wanayoishi wafugaji.

Mmoja wa wafugaji hao, Endeko Endeko alisema baadhi ya maeneo ya wafugaji hayana huduma za kijamii kama zahanati, shule, maji na umeme.