Nasa wahaha kuokoa kiapo cha Raila

Muktasari:

Japokuwa kamati ya ufundi inajaribu kutupilia mbali ripoti juu ya mgawanyiko kuhusu mpango wa kiapo hicho, vyanzo vya ndani vimefichua kwamba mazungumzo kati ya vinara hao Jumatatu na Jumanne yaliyolenga kufikia makubaliano juu ya suala hilo yalihitimishwa bila maridhiano.

Nairobi, Kenya. Muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) unakutana leo mjini Machakos katika jaribio lao la mwisho la kuwashawishi viongozi wake wakuu kuafiki mpango wa Raila Odinga kuapishwa kuwa rais wa watu Januari 30.

Japokuwa kamati ya ufundi inajaribu kutupilia mbali ripoti juu ya mgawanyiko kuhusu mpango wa kiapo hicho, vyanzo vya ndani vimefichua kwamba mazungumzo kati ya vinara hao Jumatatu na Jumanne yaliyolenga kufikia makubaliano juu ya suala hilo yalihitimishwa bila maridhiano.

Suala hilo linatarajiwa kujadiliwa upya Ijumaa katika mkutano uliopangwa katika hoteli ya Maanzoni. Baada ya hapo timu hiyo itakwenda Machakos ambako watazindua bunge la watu kwa kaunti hiyo.

Imeelezwa kwamba wafadhili na watu wenye msimamo mkali ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ndio wanasimamia kwa nguvu mkakati wa waziri mkuu huyo wa zamani aapishwe bila kujali madhara ya mgawanyiko wa ndani na kimataifa.

 

Miongoni mwa masuala moto yanayoikabili Nasa ni mahali pa kufanyia sherehe za kuapishwa kwake huku kukitarajiwa makabiliano yenye machafuko dhidi ya polisi; mashtaka yanayoweza kuwakabili Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, na majibu kutoka jumuiya ya kimataifa. Viongozi wengine wa Nasa ni Musalia Mudavadi wa Amani National Congress na Moses Wetang’ula wa Ford-Kenya.

Uongozi wa Nasa hautaki Odinga ale kiapo kwenye makazi binafsi kama alivyofanya kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye Mei 2016, kwani zoezi hilo litachukuliwa na Jubilee kama lililoshindwa.

Kwa hiyo kikao cha Maanzoni, kitajadili na kupata ufumbuzi wa masuala haya mazito ili kujiondoa kwenye kona kali ambayo upinzani umejiweka. Alhamisi kamati ya maandalizi ilisema imekamilisha mipango yote ya sherehe za kiapo cha Odinga.