Vikumbo vya urais Marekani moto

Muktasari:

Wagombea wameidhinishwa na vyama vyao

Washington, Marekani. Kumekucha nchini Marekani. Wagombea wawili wameanza kuchanja mbuga, wakijaribu kuwavutia wapiga kura.

Wanafanya kila linalowezekana kuwashawishi wananchi. Wote wameanza kukosoana hadharani huku wakianisha vipaumbele vyao.

Donald Trump aliyeidhinishwa rasmi na chama chake cha Republican wiki iliyopita ameendelea kutupa makombora kwa mpinzani wake.

Bila kukawia, Hillary Clinton ambaye ameidhinishwa na chama chake cha Democratic wiki hii amejitambulisha kama mtu wa kuwaunganisha Wamarekani.

Mgombea wa Democratic juzi alijitokeza katika mkutano mkuu wa chama hicho na kuelezea mikakati yake ya kwenda Ikulu.

Clinton mwenye umri wa miaka 68 alichukua muda mwingi wa hotuba yake kumkejeri Trump akisema mtu ambaye unaweza kumkera kirahisi na ujumbe katika Twitter.

Alisema mgombea huyo siyo mtu wanayeweza kumuamini na silaha zao za nyuklia kwani haiba yake haimuwezeshi kukabiliana na matatizo.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa moja, Clinton ameelezea mikakati yake kuhusu namna atakavyoboresha uchumi wa Marekani kwa kutoa fursa zaidi za kazi na malipo bora.

Pia, aligusia nia yake ya kuhakikisha mshikamano na kushirikisha kila upande hatua ambayo wengi wanasema ililenga kuwatuliza wafuasi sugu wa Bernie Sanders na kuwashawishi wapigakura wasioegemea vyama viwili vikuu vya upinzani.

Sera alizozigusia Clinton zimeonekana kama mwendelezo wa sera za Rais Barack Obama zikiwamo kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, kufanyia mageuzi sheria za uhamiaji, kudhibiti umiliki wa bunduki, elimu, miundo mbinu na uwekezaji.

Rais Obama, mumewe Hillary, Bill Clinton, watu mashuhuri, viongozi wa kijeshi na polisi wamemuidhinisha na kumtaja Hillary kuwa mwenye ujuzi, uwezo, ari na anayestahili zaidi kuiongoza Marekani.

Baada ya hotuba yake, katika mkutano huu mkuu wa chama cha Democratic ulioanza tangu Jumatatu, Clinton na mgombea mwenza, Tim Kaine jana walianza kampeni katika majimbo ya Pennsylvania na Ohio kwa siku tatu zijazo.

Baadaye wanatarajia kuingia kwenye majimbo mengine kabla ya kuungwa mkono na watu wao wa karibu ikiwamo familia zao.

Trump pamoja na mgombea wake mwenza pia wamekuwa wakiendelea na kampeni zao kwa kujibu hoja za wapinzani wao.

Imesalia miezi mitatu tu kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Novemba 8 kwa Wamarekani kumchagua Hillary ambaye ni mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kuwa rais au kum Donald Trump mwenye umri wa miaka 70 alisema ana uwezo wa kutatua matatizo yanayoizonga Marekani.

Licha ya Hillary kuteuliwa rasmi kuwa mgombea urais wa Marekani kupitia Democratic, ni kuwa mwanamke wa kwanza kuwania wadhifa huo na ana kazi ya kuwaunganisha wapigakura wa chama chake.

Clinton hakabiliwi na upinzani ndani ya chama chake tu bali hata katika maeneo mengine.

Kuna wasiwasi unaoonyesha wazi na Ikulu ya Marekani kuwa Urusi inajihusisha na siasa za ndani za uchaguzi huo hasa baada ya tuhuma za kuchapishwa kwa baruapepe za viongozi wa a Democratic ambazo zilionyesha njama za uongozi huo dhidi ya kampeni za Sanders.

Obama atilia shaka

Akizungumza na kituo cha televisheni cha NBC, Rais Obama alikataa kuondoa uwezekano wa uingiliaji kati wa Urusi. Licha ya kuzungumzia moja kwa moja kuhusu udukuzi huo, alisema anajua Trump amekuwa akiuzungumza vyema uongozi wa Urusi.

“Tunachojua ni kuwa Warusi wanafanya udukuzi kwenye mifumo yetu. Siyo ya Serikali pekee bali hata ya watu binafsi,” alisema.

Trump amekuwa akisema kuwa anauhusudu uongozi wa Rais Vladimir Putin wa Urusi na kuzua mashaka huenda Ikulu ya Kremlin inashiriki kumwezesha bilionea huyo kuingia Ikulu ya White House.

Hata hivyo, Ikulu ya Kremlin imetoa taarifa ya kukanusha tuhuma hizo.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisema Serikali ya Urusi imekuwa ikijiepusha na vitendo au maneno yanayoweza k utafsirika kuwa na athari kwenye mchakato wa uchaguzi wa Marekani.

Desemba mwaka jana, Rais Putin alinukuliwa akimsifia Trump kuwa ni mtu madhubuti na mwenye kipaji cha hali ya juu.