Vikundi 24 hewa vyaomba mkopo wa mamilioni

Muktasari:

Halmashauri ya Hai yavibaini, yavinyima kopo, kuvipatia vikundi 11 tu

Hai. Halmashauri ya wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, imebaini vikundi hewa 24 kati ya 35 vilivyoomba mkopo wa asilimia tano unaotolewa kwa vikundi vya akinamama na vijana kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.

Mikopo ya aina hiyo hutolewa na halmashauri zote nchini.

Akizungumza jana Ijumaa Machi 23, 2018 mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Yohana Santoo ametoa kauli hiyo katika hafla fupi ya kukabidhi hundi ya Sh30milioni kwa vikundi 11 vya wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na biashara.

Amesema kati ya vikundi 35, 24 vimeondolewa kutokana na kubainika kwamba vilifanya udanganyifu.

Amesema  baada ya kamati ya mikopo kubaini kasoro katika vikundi hivyo, wameviondoa kwa kukosa sifa.

“Tulipokea vikundi 35 kati ya hivyo vikundi 11 ndivyo vilivyoonekana kuwa na sifa ya kupewa mikopo hii, vikundi 24 vimeonekana kutokuwa na sifa,”alisema.

Mkurugenzi huyo amemwagiza ofisa maendeleo ya jamii pamoja na wataalam wake, kuhakikisha wanakwenda kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na utoaji wa mikopo na vigezo vinavyotakiwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Helga Mchomvu amesema kuwa fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani.