Tuesday, February 13, 2018

Vilio vyatanda nyumba kubomolewa Dodoma

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Vilio vimetanda baada ya Halmashauri ya Manispaa Dodoma kubomoa nyumba za makazi na biashara ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa mkoa, Dk Binilith Mahenge la kuitaka kubomoa nyumba zote zilizojengwa kiholela bila vibali vya ujenzi.

Akizungumza leo Februari 13, mmoja wa wafanyabiashara, Nassoro Masaka amesema wanashindwa kuelewa ni wapi wanakwenda baada ya vibanda vyao kubomolewa na manispaa.

“Sisi tuna familia zetu, tunawahudumia kupitia biashara hizo tunaenda wapi sasa? Tukawe wezi?”amehoji Masaka ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara walioathirika na zoezi hilo.

Mfanyabiashara mwingine, Moshi Mganda amesema amekuwa akifanya biashara ya kuuza matunda katika eneo la Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa miaka

mingi.

“Nitaenda wapi mimi? Nitaenda wapi? Mimi nina wajukuu watano ambao nimeachiwa na watoto wangu wa kike. Tutafanyaje, ninakopa nanunua matunda nauza sasa wameyaokota yote, nitaishi vipi mimi binadamu,” amesema  huku akiangua kilio.

 Justine Mbuma amesema manispaa haijajipanga na wameathirika kwa sababu wamebomolewa vibanda vya biashara na hakuna sehemu mbadala walioonyeshwa.

“Ni kweli tumepewa muda lakini tunahangaika hapa mjini hatuna sehemu ya kwenda tulitakiwa kuonyeshwa sehemu ya kwenda,” amesema.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Dodoma, Ramadhan Juma amesema zoezi hilo lililoanza jana ni endelevu na maeneo yatakayohusika ni nyumba za makazi, biashara na vibanda vya biashara.

Ameyataja maeneo ambayo hadi leo mchana walikuwa wamekamilisha kuyabomoa kuwa ni Chako ni Chako, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Majengo, Kikuyu

na Kisasa.

Amesema kesho wataendelea na maeneo mengine ambayo tayari maofisa mipango miji wameyaanisha yamejengwa kinyume cha sheria za mipango miji na wamiliki walishapewa notisi ya kubomoa kwa hiari yao,

lakini bado wameendelea kuwepo.

“Kwasasa tuko Kisasa tunabomoa nyumba zilizojengwa barabara ya Morogoro. Hawa walishalipwa fidia na mwaka jana walipewa notisi ya kuondoka katika maeneo hayo lakini hadi leo bado wapo na wengine wamepangisha kwa watu wengine,” amesema.

Akizungumzia zoezi hilo, Dk Mahenge amesema  hawawezi kufumbia macho ujenzi holela katika mji wa Dodoma kwa sababu unakwamisha uwekaji wa

miundombinu muhimu katika maeneo hayo na kwenda kinyume na sheria za mipango miji.

“Huyu wa Chako ni Chako alipewa kibali cha kufanya matengenezo ya paa, lakini yeye alipomoa paa na kuongeza sehemu na alipopewa notice (onyo)

alikataa na kuendelea kujenga,”amesema.

Hivi karibuni Dk Mahenge alifanya ziara ya ghafla katika baa iliyopo eneo la Chako ni Chako na amesema Serikali inachotaka ni kuwa na nyumba zenye sura ya makao makuu ambazo zitakuwa zimepitishwa na wataalamu wa mipango miji.

“Mkurugenzi uunde ‘task force’ itakayopitia ujenzi wote unaaondelea makao makuu kama ni halali ama sio halali na haitapendeza kuja kugundua ujenzi ukiwa umefikia hatua kubwa,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi amesema wameyapokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kwamba, kwa mujibu wa mpango

kabambe wa manispaa ya Dodoma kuanzia sasa manispaa haitatoa kibali cha kufanya marekebisho

ya paa, bali mwenye kiwanja atashauriwa kujenga ghorofa na kama hana uwezo atafute mbia.

 


-->