Viongozi, taasisi zamtumia rambirambi Rais Magufuli

Muktasari:

  • Monica amefariki leo asubuhi Agusti 19, 2018 katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa.

Dar es Salaam. Viongozi, taasisi na wanasiasa mbalimbali wamemtumia salamu za rambirambi Rais John Magufuli aliyefiwa na dada yake, Monica.

Monica amefariki leo asubuhi Agusti 19, 2018 katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa.

Salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa kupitia mitandao ya kijamii kwenda kwa Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alinukuliwa katika taarifa yake iliyosainiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akisema chama hicho kinatoa pole kwa Rais Magufuli, wana familia, ndugu, jamaa, marafiki na walioguswa na msiba huo.

“Hakuna maneno mazuri ya kuonyesha huzuni yetu katika kipindi hiki zaidi ya kusema pole sana, Mungu alitupatia dada Monica na yeye amemtwaa leo, jina lake lihimidiwe,” amesema Dk Bashiru.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika katika twitter yake akisema, “Ndugu Rais @MagufuliJP pole sana kwa msiba mliopata kwenye familia kwa kuondokewa na dada yenu Monica. Mola awape subra katika kipindi hiki kigumu.”

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas ameandika katika twitter akisema, “Natoa pole kwa Mhe. Rais @MagufuliJP kufuatia kifo cha dada yake, Monica Joseph Magufuli, kilichotokea leo. Mola awape subra.”

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameandika katika twitter yake akisema, “Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa, pole sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuondokewa na dada yako kipenzi Bi. Monica Joseph Magufuli Mwenyezi Mungu awatie nguvu familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.”

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliandika katika Twitter akiambatanisha picha ya marehemu Monica akisema, “Pole sana Mhe Rais kwa kuondokewa na dadaako!.”

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Dk Mwigulu Nchemba naye aliandika katika Twitter akiambatanisha na picha ya Monica akisema, “Pole sana Rais kwa msiba mzito wa kumpoteza Dada yetu, wewe na familia nzima tunakuombea faraja wakati huu wa majonzi, Mungu wetu wa mbinguni awatie nguvu.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeandika kwenye Twitter kikisema kinaungana na Watanzania, ndugu, jamaa na marafiki kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya Rais Magufuli kufuatia msiba wa mwanafamilia Monica Magufuli.

“Mungu awape faraja waombolezaji. Apumzike kwa amani, Amina,” kimesema

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) liliandika, “Pole sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kwa msiba huu mkubwa wa Monica Joseph Magufuli. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi.”

Chama cha waandishi wa habari wa kupinga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu Tanzania (Ojadact) waliandika katika twitter wakisema, “OJADACT, inampa pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari John Pombe Magufuli, kwa kufiwa na dada yake Bi. Monica Joseph Magufuli, aliyefariki leo kwenye hospitali ya rufaa ya  Bugando. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake litukuzwe.”