Viongozi Chadema waanza kuwasili polisi

Muktasari:

Machi 5, 2018 viongozi hao na wenzao wanne walifika kituoni hapo wakiongozwa na Dk Mashinji 

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amekuwa kiongozi wa kwanza wa chama hicho kuwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam leo Machi 13, 2018.

Mbali na Dk Mashinji, mwingine aliyefika kituoni hapo leo asubuhi ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu.

Machi 5, 2018 viongozi hao na wenzao wanne walifika kituoni hapo wakiongozwa na Dk Mashinji ambaye alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana, huku wengine alioambatana nao kutohojiwa, badala yake wote kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo leo, Machi 13, 2018.

Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.

Viongozi waliotakiwa kuripoti ni Dk Mashinji, Mwalimu na Naibu katibu mkuu Bara, John Mnyika.

Wengine ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, Mwenyekiti wa Kanda ya  Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni Mweka Hazina Bawacha.