Viongozi Chadema wakimbilia mafichoni wakihofia kukamatwa na polisi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduma, Ally Mwafongo.

Muktasari:

  • Ni viongozi wa Chadema Mkoa wa Songwe

Tunduma. Baadhi ya madiwani na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Songwe wamekimbilia mafichoni wakihofia kukamatwa na polisi.

Wameieleza MCL Digital leo Jumapili Julai 15, 2018 kuwa  wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini wanasakwa na polisi ili wakamatwe na kuunganishwa na viongozi wengine wa chama hicho waliokamatwa jana.

Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka; Katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) mkoa wa Songwe, Ayoub Sigakonamo pamoja na na wanachama zaidi ya 15, ni miongoni mwa waliokamatwa na polisi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduma, Ally Mwafongo ameieleza MCL Digital kuwa yeye pamoja na viongozi wengine wa Chadema, wakiwemo madiwani wameukimbia mji wa Tunduma baada ya kubaini kuwa wanasakwa na polisi.

Amesema wengine waliotoweka katika mji huo ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Songwe, Herode Jivava ambaye pia ni diwani wa kata ya Tunduma Mjini na mwenyekiti wa Jimbo la Tunduma, Boniface Mwakabanje.

Amesema madiwani waliopo nao mafichoni ni Quintini Kayombo (Uwanjani), Moses Mshani (Muungano) na Floini  Mwalongo (Maporomoko).

“Kama mlivyosikia Mwakajoka, katibu wa Bavicha na na wanachama wengine 15 wamekamatwa na polisi,” amesema Mwafongo.

“Tulisikia wanataka kuwakamata viongozi wote wa Chadema, tukaona isiwe tabu ngoja tuwaachie mji wafanye hicho wanachotaka kukifanya maana lengo lao ni kuona wagombea wa CCM wanapita bila kupingwa," amesema.

Amesema mvutano huo ulianza baada ya Chadema kwenda kuchukua fomu za uchaguzi na kuelezwa na msimamizi wa uchaguzi kuwa wagombea wa Chadema tayari wamechukua fomu hizo.

“Ilitushangaza maana tunaelezwa kuwa fomu zimechukuliwa na waliochukua walikuwa na utambulisho. Wagombea wetu sisi Chadema ndio tumewapitisha, ilishangaza kuambiwa kuwa kuna waliochukua fomu, hapo ndio ilianza kamatakamata,” amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduma, Castory Msigala amesema leo jioni atatolea ufafanuzi wa jambo hilo ikiwa ni pamoja na mapingamizi yaliyowasilishwa ofisini kwake.

Kuhusu Mwakajoka na wenzake, Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga amesema, “Kwa sasa tunafuatilia suala la dhamana lakini Mwakajoka na Sikagonamo wameshahojiwa.”

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema hawezi kutolea ufafanuzi suala hilo kwa njia ya simu.