Viongozi Chadema wawalaumu polisi

Muktasari:

  • Tuhuma hizo zimeibuliwa na Diwani wa Mabatini Deus Lucas (Chadema) aliyekuwa miongoni mwa viongozi walioongoza shughuli hiyo akisema licha ya kuchukua fedha zilizokuwa zimechangwa kwa ajili ya mkono wa pole kwa mwenzao, askari polisi waliohusika kwenye tukio hilo hawakuorodhesha fedha hizo kwenye fomu ya vielelezo.

Mwanza. Tukio la Jeshi la Polisi kusambaratisha mkusanyiko wa viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wakihani msiba kwa mwenzao, Laurent Chilo eneo la Mabatini jijini hapa, limechukua sura mpya baada ya kuibuka tuhuma za kukwapuliwa Sh2.5 milioni za rambirambi.

Tuhuma hizo zimeibuliwa na Diwani wa Mabatini Deus Lucas (Chadema) aliyekuwa miongoni mwa viongozi walioongoza shughuli hiyo akisema licha ya kuchukua fedha zilizokuwa zimechangwa kwa ajili ya mkono wa pole kwa mwenzao, askari polisi waliohusika kwenye tukio hilo hawakuorodhesha fedha hizo kwenye fomu ya vielelezo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kwa mujibu wa taarifa za askari wake, hakuna fedha zilizochukuliwa na kuwataka viongozi na wanachama hao kuulizana wenyewe.

“Huo ni uzushi. Labda wamegeukana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu askari wangu hawakuchukua fedha zozote eneo la tukio. Kazi ya polisi ni kulinda watu na mali zao, siyo kuiba,” alisema Kamanda Msangi.