Viongozi Geita Saccos matatani

Muktasari:

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ushindo Swalo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Kelvin Munusuri alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 6, mwaka jana kinyume na Kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11.

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Geita imewapandisha kizimbani Meneja wa Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos), Nicholaus Kamala na mjumbe wa bodi, Thobias Batiho kujibu mashtaka ya kula njama na matumizi mabaya ya madaraka.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ushindo Swalo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Kelvin Munusuri alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 6, mwaka jana kinyume na Kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11.

Katika shtaka la pili, Munusuri alidai washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kinyume na kifungu cha 31 cha sheria hiyo na kuidhinisha mkopo wa Sh10 milioni kwa mwanachama Gideon Kagoro ambaye hakuwa na vigezo vya kupatiwa mkopo.

Alidai washtakiwa hao licha ya  kufahamu Kagoro hakuwa na vigezo hivyo, waliidhinisha fedha hizo kinyume na kanuni na taratibu za mikopo ya Geita Saccos.