Viongozi mashuhuri wamzika Peres

Muktasari:

Peres amezikwa leo ikiwa ni siku tatu baada ya kufariki akiwa na umri wa miaka 93.

Rais wa zamani wa Israel, Shimon Peres amezikwa leo huku viongozi mashuhuri duniani wakimsifu  kuwa alikuwa mtu muhimu duniani.

Peres amezikwa leo ikiwa ni siku tatu baada ya kufariki akiwa na umri wa miaka 93.

Waziri Mkuu wa israel Benjamin Netanyahu amemweleza kama "mtu muhimu kwa dunia".

Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwepo kwa kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas katika mazishi hayo ni ukumbusho wa "shughuli ambayo haijakamilishwa ya kutafuta amani".

 Akihutubu wakati wa mazishi hayo, Netanyahu amesema ingawa Israel na dunia yote kwa jumla watu wanamuomboleza Peres, ameacha matumaini duniani.

"Shimon aliishi maisha yenye lengo," amewaambia waombolezaji katika makaburi ya Mlima Herzl, Jerusalem.

"Alipanda na kufikia makuu. Aligusa wengi kwa maono yake na tumaini. Alikuwa mtu muhimu kwa Israel. Alikuwa mtu muhimu kwa dunia."

'Mwenye kuota zaidi'

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, aliyesaidia kufanikisha mikataba ya amani ya Oslo kati ya Israel na Wapalestina mapema miaka ya 1990 jambo lililopelekea Shimon Peres kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, amesema kiongozi huyo alikuwa Mwisraeli "mwenye kuota zaidi".

"Alifikira sana mambo ambayo wengine wetu tungefanya. Alianza maisha kama mwanafunzi mwerevu zaidi wa Israel, alikuwa baadaye mwalimu wake bora zaidi na baada ya hapo mtu mwenye kuota zaidi."

Rais Barack Obama amemlinganisha Peres na watu wengine mashuhuri wa karne ya 20 ambao amesema alifanikiwa kukutana nao. Wengine amesema ni Nelson Mandela na Malkia Elizabeth wa Uingereza.