Viongozi wa Chadema waliokamatwa Nyasa waachiwa

Muktasari:

Taarifa ya Chadema ilieleza kuwa uamuzi wa kuwaachia huru viongozi hao ulitolewa baada ya Chadema kuzitaka mamlaka zilizohusika na ukamataji huo kuwaachia huru viongozi wao.


Viongozi wengine waliokamatwa ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, Mbunge wa Viti Maalum Ruvuma, Zubeda Sakuru, viongozi wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho mikoa ya Ruvuma na Kusini.

Dar/ Mbinga. Viongozi wanane wa Chadema akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, wameachiwa kwa dhamana, leo, saa tano asubuhi.

Viongozi hao walikamatwa Julai 15 kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali wilayani  Nyasa, Ruvuma.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu, Julai 17, na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene, imeeleza kuwa viongozi hao waliachiwa baada ya chama hicho kuzitaka mamlaka zilizohusika kuwakamata kutoa amri ya kuwaachia huru.

“Jana tulizitaka mamlaka zilizohusika kutoa amri ya kuwakamata zitoe amri ya kuwaachia huru mara moja kabla chama hakijatoa kauli nyingine kuhusu hatua zingine ambazo kingechukua kulinda sheria, uhuru na haki katika nchi,” amesema Makene katika taarifa hiyo.

Juzi Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Kamishna Gemini Mushi alizungumza na Mwananchi na kueleza kuwa viongozi hao walikamatwa baada ya kufanya maandamano wakati waliomba kibali cha kufanya kikao cha ndani.

Chama hicho kitafanya mkutano na waandishi wa habari leo saa saba mchana.