Nasa wampendekeza Ruto kugombea urais 2022

Muktasari:

Waliomwidhinisha Ruto ni Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja na wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Jones Mlolwa (Voi), Ali Mbogo (Kisauni) na Danson Mwashako (Wundanyi)


Nairobi, Kenya. Kikundi cha viongozi kutoka ukanda wa pwani washirika wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) Jumapili walimwidhinisha Makamu wa Rais William Ruto kuwa mgombea urais mwaka 2022.

Akizungumza wakati wa harambee katika Kanisa la Mtakatifu Barnabas la Anglikana Voi, kaunti ya Taita Taveta walisema hakuna mgombea bora wa kuwaongoza Wakenya.

Waliomwidhinisha Ruto ni Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja, na wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Jones Mlolwa (Voi), Ali Mbogo (Kisauni) na Danson Mwashako (Wundanyi).

Jumwa ambaye alikuwa mkosoaji mkali wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Ruto, na ambaye amekuwa mpinzani mashuhuri, alisema wakati wa mapambano ya kisiasa umekwisha.

"Hatuwezi kuacha wazo ambalo muda wake umefika. Mwaka wa 2022 hakuna mgombea mwingine wa urais isipokuwa naibu rais," alisema mwanamama huyo.

Jumwa alisema upinzani utasimamia hoja kubwa nne za Jubilee.

Alisema wazi wakuu wa Nasa kwamba wanajaribu kupotosha mazungumzo kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

"Ikiwa kweli ni wamoja basi hakuna haja ya wao kututishia dhidi ya kuungana na serikali," alisema mbunge huyo.

Alisema kuwa migawanyiko ya kisiasa haitaleta maendeleo kwa wananchi, lakini itasaidia kuwagawa Wakenya kwa misingi ya ukabila.

"Kilichotokea kama maji yapitayo chini ya daraja. Ni lazima tukubali mabadiliko na kuunga mkono viongozi wetu ambao wameamua kuungana kwa ajili ya nchi," aliongeza.

Mbunge wa Voi, Jones Mlolwa alisema injili iliyohubiriwa na upinzani 'kataa' ilihitimishwa Rais na Odinga walipokubaliana kujadili.