Viongozi wa dini, siasa wanusa hofu

Muktasari:

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni na Siha ambapo CCM ilishinda, huku kukitokea mauaji ya mtu mmoja jijini Dar es Salaam kutokana na mapambano kati ya waandamanaji na polisi

Viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini wameitaka Serikali kuweka mfumo shirikishi katika utawala ili kuondoa hofu ya usalama iliyojitokeza kutokana vurugu, mauaji na ukandamizwaji wa demokrasia.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni na Siha ambapo CCM ilishinda, huku kukitokea mauaji ya mtu mmoja jijini Dar es Salaam kutokana na mapambano kati ya waandamanaji na polisi.

Wakizungumza jana katika kongamano la viongozi wa madhehebu ya dini na vyama vya siasa lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam, baadhi ya viongozi walitaka amani ilindwe, lakini pia demokrasia iheshimiwe. Amir wa Shura ya Maimamu, Alhaj Sheikh Musa Kundecha alisema hali ya hofu inatokana na nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi kwa wafuasi wa vyama vya siasa.

“Suala la hofu ni hali halisi. Kwenye mfumo wa siasa tulizoea kuona watu wanasambazwa kwa mabomu ya machozi, leo wanasambazwa kwa risasi za moto, ni hatari kweli. Unapambanaje na watu wasio na silaha kwa risasi za moto na wale ni raia?” alihoji. Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera akitoa mfano wa hatua ya polisi kuwatawanya waandamanaji kwa risasi za moto.

“Hofu ipo kwa sababu kwa uhai wangu niliokuwa nao hapa nchini sijawahi kuona risasi za moto zinarushwa kwa raia wasiokuwa na silaha. Vyama vingi vimeanza mwaka 1992, walikuwepo kina Mrema (Augustine) tulikuwa tunawasukuma kwenye magari, yalikuwa yakitumika mabomu ya machozi, sasa leo kwa nini watumie risasi?” alihoji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisisitiza hoja hiyo akisema tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 nchi imetikiswa. “Taifa hili limetikiswa kwa kiwango kikubwa. Haki ya kuzungumza haipo, haki ya kukusanyika haipo. Taasisi ya haki za binadamu iko wapi? Hatuioni ikisema, imekaa kimya,” alisema Mrema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alipinga kuwepo kwa hofu nchini akisema Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani.

“Watu wanaandamana haiashirii amani, tunapoona watu wanakaidi amri halali ya polisi pia haiashirii amani,” alisema Cheyo.