Viongozi wa dini, taasisi watoa wito wa amani, uchunguzi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye moja ya makaburi la watu waliokufa kwenye ajali ya kivuko cha Mv Nyerere, aliposhiriki mazishi yaliyofanyika eneo la Ukara, Mwanza jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Mahimbo Mndolwa mbali na kutoa pole, amewataka waumini wa dini zote kuwaombea waliopoteza maisha.

Dar es Salaam. Siku nne baada ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali wameendelea kutoa matamko wakiwataka Watanzania kuwa kitu kimoja sambamba na kuchukuliwa hatua kwa waliohusika na ajali hiyo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Mahimbo Mndolwa mbali na kutoa pole, amewataka waumini wa dini zote kuwaombea waliopoteza maisha.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Mndolwa aliwataka Watanzania kuondoa tofauti zao, kuungana kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki.

“Kanisa la Anglikana linawatia moyo na kuwoamba wote kuwa na subira na kumtegemea Mungu. Hiki si kipindi cha kulaumiana, bali kila mmoja anapaswa kujitolea kwa hali na mali kuhakikisha shughuli za uokoaji pamoja na kuzika miili ya waliokufa zinafanyika bila vikwazo,” alisema.

“Wakati tukitoa machozi kuwalilia ndugu zetu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya majini, tuelekeze mioyo yetu kwa Mungu tukiamini kwamba yeye ndiye aliyetuletea msiba huu na ndiye atakayetuletea faraja.”

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo alituma salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli akisema msiba huo ni wa Taifa.

Dk Shoo alisema kanisa hilo lipo pamoja na Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

“Nitumie fursa hii kumpa pole Rais wetu kwa kuwa huu ni msiba wa kitaifa na tuko pamoja katika maombolezo haya,” alisema, “Manusura wa ajali hii tuzidi kuwaombea, Mungu awape uponyaji wa haraka. Poleni Watanzania wenzangu na Mungu azidi kuibariki nchi yetu.”

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa pole kwa Rais Magufuli, familia za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki.

Katika taarifa yake iliyotiwa saini na kaimu mwenyekiti wake, Deodatus Balile, TEF imeisihi Serikali, wananchi na wadau mbalimbali kuongeza elimu ya udhibiti wa majanga, kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa usalama wa abiria.

“Tunaamini utafanyika uchunguzi wa kina na waliohusika na uzembe huu uliogharimu maisha ya Watanzania watafikishwa katika vyombo vya sheria,” inaeleza taarifa hiyo.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeiomba Serikali kufuatilia sababu za ajali hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TGNP, Lilian Liundi jana imeeleza kuwa kuna haja ya kuweka mikakati thabiti ya kuhahakikisha ajali za majini zinakoma ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.

Mtandao huo umeitaka Serikali kuweka mifumo endelevu ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa vyombo vya moto na kuongeza bajeti ya huduma muhimu katika maeneo ya visiwani.