Viongozi wa dini, wanasiasa waja na dawa kushamirisha demokrasia

Muktasari:

Safari hii viongozi hao wamekutana chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na baada ya majadiliano wakaibuka na ushauri wa pamoja unaoitaka Serikali pamoja na mambo mengine kufufua mchakato wa Katiba na kujenga mfumo wa siasa shirikishi miongoni mwa wadau.

Hakuna ubishi kwamba yapo malalamiko juu ya uendeshaji wa siasa nchini. Madai haya yamekuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na pia viongozi wa dini.

Safari hii viongozi hao wamekutana chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na baada ya majadiliano wakaibuka na ushauri wa pamoja unaoitaka Serikali pamoja na mambo mengine kufufua mchakato wa Katiba na kujenga mfumo wa siasa shirikishi miongoni mwa wadau.

Hoja za zinazowasukuma viongozi hao kukaa na kutoka na mapendekezo hayo ya pamoja, zinatokana na hatua ya Serikali kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano, jambo linaloelezwa linakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni.

Vilevile, katika mkutano wa hivi karibuni, viongozi hao wamejadili matukio yanayotia hofu ya mauaji ya watu mbalimbali yanatokea nchini, miili ya watu kuokotwa katika fukwe za bahari, watu kutekwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mkutano huo wa TCD umefanyika wakati tukio la kuuawa kwa risasi kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini likiwa limechukua nafasi. Pia, ilikuwa siku chache baada ya kuuawa kiongozi wa Chadema katika Kata ya Hananasif na kuleta sintofahamu kubwa.

Mjadala wa masuala hayo umekuwa mkubwa katika mkutano huo ambao lengo lake lilikuwa kujadili lengo la 16 la malengo ya maendeleo endelevu ya milenia linalosisitiza, “Kuendeleza jamii jumuishi na yenye amani kwa ajili ya maendeleo endelevu, kutoa haki kwa wote na kujenga taasisi imara zenye kuwajibika katika nyanja zote.”

Akifafanua kuhusu lengo hilo, Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia anasema mkutano huo licha ya kujadili lengo la 16 la maendeleo endelevu, umejikita kwenye Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1947.

Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo anasema wamejadili kwa kiasi gani mfumo wa vyama vingi umeimarika tangu uliporejeshwa mwaka 1992, kuimarika kwa mihimili mitatu ya dola – Bunge na Mahakama na Serikali.

“Tumetazama Serikali mifumo yake iko imara kiasi gani? Miaka 56 ya Uhuru taasisi zake za kiraia ziko kiasi gani? Uimara wa mahakama, Bunge liko imara kiasi gani? Sisi tuna katiba, je uimara wa Katiba yetu ambayo ni sheria mama, ukoje?” anasema Mbatia huku msisitizo mkubwa ukiwa ni Katiba Mpya kama mwarobaini ya sehemu kubwa ya matatizo.

Hata hivyo, wakati viongozi hao wakitaja suala la Katiba Mpya na umuhimu wake, mwakilishi wa CCM katika mkutano huo, Wilson Mukama anasema suala la Katiba kwa chama hicho halijapuuzwa bali utawala uliopo una vipaumbele vyake unavyovitekeleza kwanza.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

“Rais aliyepo ana ‘priorities’ zake sasa. Anataka kujenga nchi katika kipindi kifupi hiki, kupambana na umaskini, kujenga uchumi. Kwa hiyo ni vipaumbele tu, siyo kwamba amepuuza, kwa sababu huo ni uamuzi wa msingi wa nchi. Ni uamuzi ulioungwa mkono na rasilimali za Taifa zimetumika,” anasema Mukama na kuongeza:

“Rais (Jakaya) Kikwete ndiye aliyeanzisha mchakato, lakini haukufika mwisho. Wataalamu wanatuambia unaweza kutumia mazingira kutengeneza historia, lakini wewe huwezi kulazimisha mazingira kutengeneza historia unayotaka.”

Hata hivyo, Mukama aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM anasema Katiba mpya siyo suluhisho la kutengemaa kwa nchi.

“Hata Katiba mkiwa nayo, kwa mfano Katiba ya Kenya ni nzuri sana, lakini mbona wana marais wawili? Kwa hiyo kufikiri kwamba Katiba ndiyo determinant (kigezo), hapana. Ndiyo maana lengo la 16 linasema kuwa na jamii jumuishi?

Kuhusu ujenzi wa taasisi imara, Mukama anatolea mfano wa CCM akisema imejengekea kuwa taasisi imara, kuliko vyama vya nchi nyingine za Afrika vilivyoishia kujenga viongozi wababe.

“Obama (Barrack, Rais mstaafu wa Marekani) alipokwenda Ghana kwa mara ya kwanza, alisema Afrika inahitaji viongozi wababe au taasisi imara? Taasisi imara zinawezesha kurithishana uongozi, umoja wa kitaifa. Lakini mabwana wakubwa kama kina Mobutu, Idd Amin wameacha nini?” alihoji.

“Nimetoa mfano wa CCM, walioianzisha kina Mwalimu Nyerere, wameshakwenda, lakini ina utaratibu wa kutengeneza viongozi wake wapya. Aliondoka Mwalimu akaja (Ali Hassan)Mwinyi, amekuja (Benjamin) Mkapa ametoka, amekuja Kikwete naye ameondoka. Kwa hiyo, huwezi kuwapata viongozi kidemokrasia nje ya mfumo wa taasisi,” anasema Mukama.

Mapendekezo mengine

Akisoma mambo waliyokubaliana katika mkutano huo, Mbatia anasema mbali na kuamua kusisitiza mchakato wa mabadiliko ya Katiba urejeshwe upya, pia walipendekeza kuboresha kituo cha demokrasia kama jukwaa la majadiliano.

Hata hivyo, ukali wa meno ya mkutano huo unaishia katika kushauri. Hivyo mkutano huo kwa mujibu wa Mbatia, uliafikiana kuomba kukutana na Rais John Magufuli ili kuwasilisha kwake mapendekezo hayo.

“Tumeona ipo haja ya kujenga taasisi imara zitakazoleta utengamano wa kitaifa, weledi usawa na haki, anasema Mbatia akisisitiza kuwa umoja wa kitaifa utajengwa kwa kuondoa dosari zilizoleta migogoro hivi karibuni na maendeleo endelevu yataletwa kwa kuondoa siasa za chuki nchini.

Mbatia anasema mkutano unashauri uhuru wa kutoa amani uheshimiwe na wadau wa siasa wajiepushe na siasa za chuki.

Usimamiaji mapendekezo

Ili kusimamia utekelezaji wa mapendekezo hayo, Mbatia anasema watayapeleka kwa kila chama cha siasa kinachounda taasisi hiyo ili yajadiliwa kwa kina kisha yatapelekwa kwenye mkutano mkuu wa TCD kwa ufuatiliaji zaidi.

Mapema kabla ya mkutano, wajumbe kila moja alikuwa na maoni yake binafsi kuhusu hali inayoendelea hapa nchini hasa kuhusu demokrasia na usalama, jambo ambalo baadhi ya viongozi wa dini na siasa wanasema linasuasua na kusababisha wananchi kuishi kwa hofu.

Amiri wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania, Alhaj Sheikh Musa Kundecha anasema hali ya hofu inatokana na nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi kwa wafuasi wa vyama vya siasa.

“Suala la hofu ni hali halisi. Kwenye mfumo wa siasa tulizoea kuona watu wanatawanywa kwa mabomu ya machozi leo wanatawanywa kwa risasi za moto ni hatari kweli. Unapambanaje na watu wasio na silaha kwa risasi za moto na wale ni raia?” anahoji Sheikh Kundecha.

Kuhusu demokrasia, anasema vyama vya upinzani wakati vipo kisheria lakini vimekuwa na wakati mgumu kufanya siasa.

Pia, anagusia suala la viongozi kuhama vyama vyao wakidai kuunga mkono juhudi za Serikali, “Utamsikia kiongozi anasema hao wapinzani msiwasikilize wahuni, hao siyo watu wazuri, wataleta mambo kama ya Rwanda. Yaani ni kama watu wa mtaani wamezuka wanadai siasa. Hayo ndiyo tunayaona leo,” anasema na kuongeza:

“Leo kumekuwa na jitihada za kumtoa kiongozi huku na kuingia huku. Siyo kila ukikubali ni kuridhika na lile jambo. Waswahili wanasema, mkono usioweza kuuvunja, basi ubusu. Watu wanaweza kwenda kule siyo kwa sababu wanalazimika, hawana njia ya kufanya, lakini siyo ishara kwamba wamekubali,” anasema.

Kauli hiyo pia inaungwa mkono na Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera akitoa mfano wa hatua ya polisi kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi na risasi.

“Hofu ipo kwa sababu kwa uhai wangu niliokuwa hapa nchini, sijawahi kuona risasi za moto zinarushwa kwa raia wasiokuwa na silaha. Vyama vingi vimeanza mwaka 1992, walikuwapo kina (Augustine) Mrema, tulikuwa tunawasukuma kwenye magari, yalikuwa yakitumika mabomu ya machozi, sasa leo kwa nini watumie risasi?” alihoji Askofu Bagonza.

Anasema kinachohitajika kwa sasa ni kuwa na siasa shirikishi bila kujali jinsia na vyama vya siasa.

“Hii habari ya chama kimoja kinaruhusiwa kufanya mambo yote na vingine viko kimya nafikiri siyo sawa. Tunahitaji siasa za kujumuisha watu wote bila kujali tofauti zao. wanawake wanaume washiriki katika siasa za nchi,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa oganaizesheni na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema anasisitiza hoja hiyo akisema tangu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchi imetikiswa.

“Tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, taifa hili limetikiswa kwa kiwango kikubwa. Haki ya kuzungumza haipo, haki ya kukusanyika haipo. Taasisi ya Haki za binadamu iko wapi, hatuioni ikisema, imekaa kimya,” anasema Mrema.

Huku akihoji sababu za vyombo vinavyosimamia haki kutochukua hatua huku mihimili ya nchi ikitikiswa.

“Ukiangalia Bunge nalo limetikiswa, bahati mbaya hatujui linafanya nini kwa sababu halionekani. Imebaki Serikali, chaguzi haziendeshwi kwa haki. Hali ni mbaya kuliko tulikotoka,” anasema.

Hata hivyo, akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo anapinga kuwapo kwa hofu nchini, akisema Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani.

“Kitu ambacho ninachokiona, Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani. Hali tunayoiona, watu wanaandamana, haiashirii amani, tunapoona watu wanakaidi amri halali ya polisi, pia haiashirii amani,” anasema Cheyo.

Maaskofu pia walizungumzia hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka wazi mali na madeni ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship linaloongozwa na Zachary Kakobe hivi karibuni, baadhi wakiitaka mamlaka hiyo kufuata maadili yake ya kazi.

Askofu Bagonza anasema hatua hiyo haikuwa nzuri na haikubaliki kwa taasisi za dini.

“Hiyo ni mbaya sana. Kama Askofu Kakobe asingesema kile alichosema asingechunguzwa. Kwa hiyo kama hutaki kuchunguzwa usiseme kitu? Kwa hiyo maisha yetu yanakwenda mbali hadi kwenye mali za kanisa,” anahoji Askofu Bagonza.

Kauli hiyo inaunga mkono na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Alinikisa Cheyo akitaka TRA ifuate maadili ya kazi.

“Nafikiri TRA wanayo maadili yao wanaposhughulika na wateja wao. Huwezi kuweka wazi madeni na mali za mteja wako vile. Siyo makanisa tu hata wateja wa kawaida, labda ni kwa sababu ya mlolongo wa yaliyotokea. Ni bvizuri TRA wafuate maadili ya kazi yao,” alisema Dk Cheyo.