Viongozi wa dini na ukimya wa kobe

WATANZANIA WATAKIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUSHUKURU KWA KILA JAMBO

Muktasari:

Kumbe viongozi wa dini ya Kikristo walikuwa wameinama makusudi “wakitunga sheria” kama afanyavyo kobe.

Upo msemo wa wahenga kwamba “ukiona kobe kainama ujue anatunga sheria”. Ndivyo unavyoweza kutafsiri ukimya wa viongozi wa dini siku za hivi, uliosababisha watupiwe lawama kuwa kushindwa kukemea vitendo ambavyo watu hao wanatafsiri kuwa ni ukiukwaji wa Katiba, sheria na haki za wananchi.

Unaweza kusema ukimya huo ulioibua manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa, umetoweka kuanzia Desemba 24, mwaka jana. Kumbe viongozi wa dini ya Kikristo walikuwa wameinama makusudi “wakitunga sheria” kama afanyavyo kobe.

Siku hiyo wakati wa mkesha wa Krismasi katika makanisa mbalimbali walianza kama ilivyo kawaida kwa sikukuu zote za aina hiyo, kwa kuhimiza amani, upendo, kukemea maovu na kuhitimisha kwa kuwashauri viongozi wa Serikali “kukubali kushauriwa na kutominya uhuru wa watu kutoa maoni”.

Hawakuishia hapo, kama vile walikuwa wamepigiana simu, waliendelea kuonya kuhusu masuala hayo siku iliyofuata yaani Krismasi yenyewe na kama vile haitoshi, baadhi yao walitoka makanisani hadi kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na kutoa yao ya moyoni.

Mwenendo huo uliinyanua Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira kuandika waraka wa kuwataka viongozi hao kutojihusisha na masuala ya siasa, bali wajikite kuzungumzia mambo yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao, vinginevyo zitafutwa.

Ujumbe wenyewe

Akiwa katika ibada ya mkesha na baadaye ile ya Sikukuu ya Krisimasi katika Usharika wa Moshi Mjini, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo alisema Watanzania hivi sasa wanajengewa hofu ili wasiseme ukweli wa kile wanachokiamini.

“Kuna watu wanajaribu kuwajaza watu hofu ili wasiseme ukweli na wasikae katika kweli. Watu wanajazwa hofu ili wasitetee kile wanachokiona ni cha haki.

“Watu wanajazwa hofu ili wasiwe huru kutoa mawazo yao wanavyojisikia kuhusu Kristo, nchi yao na imani yao. Tukidumu katika kweli inatupa nguvu na uhuru wa kusema na kutembea bila woga.”

Mbali na ujumbe huo, Askofu mwenzake Isaac Amani Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi akagusia matukio yaliyotikisa nchi mwaka jana ya kutoweka kwa watu na mauaji ya kikatili kwa wasio na hatia aliyosema ni ishara mbaya kwa Taifa.

Alisema Tanzania ya leo si ya miaka ya nyuma kwa kuwa watu wamekuwa na hofu kutokana na vitendo hivyo viovu.

Anasema hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda amani kwa kuwa vitendo vya kutoweka kwa watu na mauaji yanayoendelea nchini yanaleta hofu kwa wananchi.

Kana kwamba maaskofu hao walikuwa wameambizana, Askofu wa Anglikana Zanzibar, Michael Hafidhi naye akaibuka kwa upande wake akiwataka viongozi wa Serikali kukubali kushauriwa na viongozi wa dini ili kuleta maendeleo.

Alisema kuzaliwa kwa Yesu kulileta mtafaruku kwa mtawala aliyeitwa Herode ambaye baada ya kushauriwa vibaya, aliamuru watoto walio chini ya miaka miwili wauawe ikiwa ni mpango wa kumuua mtoto Yesu.

Akifafanua suala hilo baada ya ibada hiyo, Askofu Hafidhi anasema kumekuwa na urasimu kwa viongozi wa Serikali kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini.

“Tunawashauri kwa maendeleo ya jamii, si mambo mengine. Kwa sababu usitegemee mimi nitakuwa Rais au waziri mkuu. Nafasi ya kuwashauri imekuwa ngumu mno kwa sababu ya urasimu wa watu wa chini. Viongozi hawana shida ila ule urasimu, inakuwa shida.”

Katika mfululizo wa salamu hizo, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani alionya kuhusu viongozi kujifanya miungu watu badala ya kushuka kwa wananchi na kuwatumikia.

Alisema imekuwa ni tabia kwa wanasiasa wengi kufika kwa wananchi hasa kipindi cha uchaguzi lakini wanapochaguliwa husahau kuwatumikia.

Wakati viongozi hao wakielekeza ujumbe wao kwa viongozi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo yeye aliwageukia wananchi, akisema ili kupata amani ya kweli duniani, wasitegemewe viongozi waliopo madarakani, bali wao wenyewe.

Anasema kila mtu anapaswa kufahamu kuwa chimbuko la amani ni kufanya kazi halali inayopendeza machoni pa Mungu.

Hata hivyo, alisema mifumo ya kiutawala ya binadamu inapaswa kuzingatia maadili na kwamba, mikakati inayofanywa na viongozi inatakiwa kutosahau hilo.

“Tunaweza kufanya hivyo tukajikuta katika makosa yaliyoangusha mataifa mengi, tujaribu kuepuka hilo, ndiyo maana binafsi nafarijika kumsikia Rais na wasaidizi wake wanapoongelea kuhusu maadili,” alisema Kardinali Pengo.

Mbali na masuala ya demokrasia a uhuru wa maoni, yapo mambo mengine yaliyowagusa viongozi hao kama Askofu, Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anayezungumzia uchumi na hali ya umaskini.

Anasema licha ya kuwapo kwa taarifa za uchumi wa nchi kukua, bado kuna hali ya umaskini kwa wananchi huku baadhi ya viongozi wakizidi kuwa matajiri.

Anawataka viongozi wasitumie nafasi zao kujilimbikizia mali wakati wananchi wengi wakizidi kuwa maskini, lixcha ya kuwa inaelezwa uchumi wa nchi unapanda kwa asilimia saba.

Ujumbe mitandoni

Siku mbili baada ya Krismasi na mahubiri hayo kuibua mjadala, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kuhoji mipaka ya kuzungumzia masuala ya siasa na dini, lakini msisitizo wake ukiwataka wananchi kutojengewa hofu ya kutoa maoni yao.

Katika ujumbe huo uliosambaa kwa wiki, Askofu Bagonza anasema, “Wakijenga shule hawaingilii wizara ya elimu, wakijenga hospitali hawaingilii wizara ya afya, wakijenga kisima cha maji hawaingilii wizara ya maji. Wakiombea mvua hawaingilii mamlaka ya hali ya hewa.

Akaongeza, “Wakihimiza kilimo hawaingilii wizara ya kilimo, wakitoa msaada wa dawa kwa mgonjwa, wanapongezwa, wakihoji kwa nini hakuna dawa hospitali, wanaambiwa wanachanganya dini na siasa na wakikosoa mfumo wa kisiasa, wanaambiwa wanaingilia siasa. Kuna kitu hakiendi sawa.”

Katika ufafanuzi wake “Tujenge utamaduni wa kujenga hoja na kutotukanana matusi. Kuna watu wengine wanaamini uhuru wa kusema umetoweka. Nasema, kuwapa uhuru watu kusema na kutoa mawazo yao kunajenga kuliko kuwazuia au kuwajengea hofu.”

Askofu Bagonza pia anajibu madai kwamba viongozi wa dini wamekuwa wakimya sasa, “Si kama huko nyuma, tulikuwa tunasema na sasa hatusemi, hapana. Krismasi hii tumeanza kusema, lakini tukisema mnasema tunasema sana, tukikaa kimya mnasema tunakaa kimya.”

Kakobe aibuka

Baada ya kimya cha muda mrefu, Krismasi hii pia ilimuibua Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe akikosoa namna Serikali inavyotenda mambo yake, akidai kwamba Tanzania si nchi ya chama kimoja kama ambavyo viongozi wanataka kuigeuza na hivyo kuwataka viongozi wa Serikali waanze kutubu.

Ujumbe wafika serikalini

Kama ishara ya ujumbe wa viongozi hao kufika serikalini, Meja Jenerali Rwegasira aakatoa tamko akisema viongozi wa dini wanapaswa kujikita kuzungumzia masuala ya dini yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao na kuachana na ya kisiasa, vinginevyo zitafutwa.

Ametaja moja kwamoja kauli za viongozi hao wakati Krismasi, anasema kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya ukiukwaji wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Jumuiya zilizoundwa chini ya sheria ya Jumuiya, inayotamka pamoja na mengine kuwa Jumuiya yoyote.

Baadaye katibu mkuu huyo wa wizara akifafanua kuwa anachozungumzia yeye ni ukosoaji, lakini viongozi wa dini wakiisifia Serikali au viongozi wake hawatakuwa wametenda kosa lolote.

“Mimi sioni kama ni kosa, unapozungumza mambo yanayoleta umoja hakuna kosa ila kukosoa viongozi, kuwakashifu hatuwezi kukubali,” Anasema.

Je kusifia ni moja ya mambo ya siasa?

“Ninaloangalia ni je, wanachosema kinaleta mtafaruku katika jamii, lakini kama unazungumza au kuhamasisha amani hilo si tatizo,” anajibu Meja Jenerali Rwegasira.

Tofauti ya siasa na maisha ya kawaida

Kuhusu kutofautisha siasa na maisha ya kawaida na hasa kwa viongozi wa dini anaesema, “Ujue siasa ni kila mtu anavyoitafsiri, mfano unaweza kuwa unazungumza na watu ukasema uongo, utasikia wanasema hizo siasa sasa.”

Awali, Rwegasira akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) kuhusu onyo la Serikali alisema, “Kama Serikali inakwenda vibaya watumie majukwaa yao kuzungumza na si kutumia nyumba za ibada yanayounganisha waumini kuzungumza siasa na tulichokifanya sasa ni kuwakumbusha tu na hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua,” alisema.

Kauli za wanasiasa

Mjadala huo haukuishia makanisani wala serikalini, uliwaibua hata wanasiasa. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amasema viongozi wa dini wanapaswa kuachwa waikosoe Serikali.

“Kesho tutazitaka taasisi za dini zihamasishe amani, maendeleo, zipongeze ‘Its important’ (ni muhimu) kukubali kukosolewa,” anaandika Bashe katika akaunti ya Twitter.

Anasema Serikali haipaswi kufanya hivyo ikiwa taasisi za dini hazivunji sheria. “Taasisi za dini zina haki kutoa maoni yake juu ya siasa, uchumi na masuala yote ya kijamii, viongozi wa dini wana nafasi yao.”

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam kuhusu onyo hilo anasema si kweli kwamba wamezuiwa lakini wajaribu kutumia lugha za staha na kutokutoa kauli kamilishi zisizokuwa na ushahidi.

“Wako wazi kusema chochote kwa mujibu wa Katiba za nchi na sheria zetu. Anayesema mtu kazuiliwa uhuru wake wa maoni atakuwa na matatizo mengine, ninachokifahamu kuzungumza kauli za matusi ni makosa,” anasema Polepole.

Mjadala huo mzima umebadili mada, ukimya wa viongozi wa dini umegeuka na kuwa kauli za kutikisa. Kumbe walikuwa wameinama wanatunga sheria.