Viongozi wa dini wataka umakini vita dawa za kulevya

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Padri Solomoni aliwataka viongozi wanaochunguza suala hilo kuwa makini ili wasiharibu haki ya mtuhumiwa.

Dar es Salaam. Katibu wa baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya nchini, Padri John Solomoni ameitaka Serikali itekeleze kwa ufasaha suala la kupambana na dawa za kulevya ili lisije kuleta maumivu kwa raia ambao hawana hatia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Padri Solomoni aliwataka viongozi wanaochunguza suala hilo kuwa makini ili wasiharibu haki ya mtuhumiwa.

Alisema uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya ni janga ambalo linahitaji viongozi wanaopambana nalo kuwa makini kwani linahusisha wasanii, wafanyabiashara na viongozi wa dini ili lisije kuondoa heshima zao baadaye.

“Ikumbukwe kwamba wanaotajwa ni watuhumiwa, huenda baada ya uchunguzi wakabainika kuwa hawakuhusika... baada ya kugundulika kuwa hawana hatia na itakuwa ngumu kurudisha aliyokuwa nayo hapo mwanzoni,” alisema.

Pamoja na kupongeza jitihada zilizoonyeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda za kupambana na matumizi ya dawa hizo, ameshauri vita hiyo iwe endelevu na isifanyike katika mkoa mmoja pekee.

“Tuungane kwa pamoja kupiga vita biashara na utumiaji wa dawa za kulevya ili Taifa lisiangamie na biashara hii haramu,” alisema Padri Solomoni.

Akizungumza katika mkutano huo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum alisema baraza hilo litahakikisha kuwa linaunga mkono juhudi zifanywazo na Serikali kupambana na jambo hilo.

“Suala la matumizi ya dawa za kulevya limekuwa kikwazo cha maendeleo nchini kutokana na nguvu kubwa ya Taifa ambayo ni vijana kujihusisha na utumiaji wa dawa hizo,” alisema.

Alisema baraza linawataka viongozi wengine kuiga mfano wa Makonda wa kupambana na uovu wa uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambao ni janga kwa Taifa.

“Tunawaomba wananchi wote kuunga mkono suala hili pamoja na kuonyesha ushirikiano wa kutosha kwa wale walioamua kujitoa kwa ajili ya nchi yetu.”