Viongozi wakuu Chadema njiani kuelekea Polisi

Muktasari:

Viongozi walioitwa na Mambosasa ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu wakuu (bara), John Mnyika na Salum Mwalimu (Zanzibar).


Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi saba wa Chadema  wanaelekea Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito wa kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 20, 2018 mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema viongozi hao wanajiandaa muda huu kuelekea kituoni.

Viongozi walioitwa na Mambosasa ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu wakuu (bara), John Mnyika na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Pia wamo, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Ester Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Jana, Mambosasa aliieleza MCL Digital kuwa viongozi hao ni watuhumiwa na kama wameitwa polisi ni fadhila tu, ila kwa yaliyotokea wanapaswa kukamatwa.

Wito wa viongozi hao polisi umekuja siku siku nne tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usfairishaji (NIT).

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.