Wednesday, August 16, 2017

Viongozi wapya Talgwu wanolewa Pwani

By Sanjito Msafiri,Mwananchi mwananchipapers@mwananchi .co.tz

Viongozi  wapya 70 kutoka matawi 40 ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu) mkoani Pwani wamepata mafunzo yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa wanachama wao kwa kufuata misingi inayokubalika.

Mada zilizotolewa kwenye mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamefanyika wilayani hapa kati ya Agosti 15 na 16 ni namna ilivyo na utendaji kazi wa Sheria ya Kazi namba 6 ya mwaka 2004 na sheria namba 8 ya mwaka 2002 pamoja na umuhimu wa vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Katibu wa Talgwu mkoani Pwani, Amina Darabu amesema lengo ni kuwajengea uwezo zaidi ili wapate mbinu za utendaji kwa kuwa msingi wa vyama vya wafanyakazi uko kwenye ngazi ya matawi ambako wao ndio wasimamizi.

"Wengi wa washiriki wa mafunzo haya ni viongozi wapya wa matawi na sisi Talgwu tunasimamia haki za wafanyakazi wa Serikali za mitaa,” amesema na kuongeza kuwa:

“Pia, watatatua migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza baina ya waajiri na waajiriwa, hivyo ni matumaini kuwa baada ya mafunzo haya wataenda kutekeleza majukumu yao kama inavyostahili huko matawini."

Mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Musa Gama amewataka viongozi hao kwenda kusimamia majukumu yao kwa kufuata haki pamoja na kutoa elimu kwa wanachama wao.

"Ni lazima ieleweke kuwa mnapofanya kazi mnatakiwa mfanye kwa uwazi, hususan kwa upande wa masuala yanayohusu pesa kile mtakachokitekeleza kinatakiwa kitekelezwe kwa ubora kulingana na thamani halisi ya pesa na si vinginevyo,"amesema.

-->