Viongozi watatu wa Chadema wafungwa

Muktasari:

Mathew ambaye pia aligombea ubunge wa Mtama katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na mwenzake, katibu wa Chadema tawi la Nyangamala, Lindi, Ismail Kupulila walihukumiwa kifungo cha miezi minane kila mmoja kwa kosa la kufanya mikusanyiko bila kibali.

Lindi/Tarime. Viongozi watatu wa Chadema akiwamo mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Lindi, Suleiman Mathew wamehukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia kwa makosa tofauti.

Mathew ambaye pia aligombea ubunge wa Mtama katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na mwenzake, katibu wa Chadema tawi la Nyangamala, Lindi, Ismail Kupulila walihukumiwa kifungo cha miezi minane kila mmoja kwa kosa la kufanya mikusanyiko bila kibali.

Kiongozi mwingine wa Chadema aliyehukumiwa ni Diwani wa Kyangasaka, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mustapha Sanya ambaye amefungwa miaka mitano kwa kosa la kutumia madaraka vibaya na kughushi nyaraka.

Lindi

Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Lindi, Godfrey Mhini aliwahukumu Mathew na Kupulila baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka.

Licha ya Hakimu Mhini kutoa hukumu ya kesi hiyo namba 36/2016, chini ya kifungu cha 74 (1) na 75 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, aliweka wazi nafasi ya washtakiwa kukata rufaa iwapo wataona hawakuridhika.

Washtakiwa wengine wanne katika kesi ambao ni wanachama wa Chadema, Bashiru Rashidi, Hassani Mchihima, Abdalaah Masikini na Mohamedi Makolela wote wakazi na wakulima wa Kata ya Nyangamala waliachiwa huru baada ya makosa dhidi yao kushindwa kuthibitika.

Awali, Wakili wa Serikali, Juma Maige aliiambia mahakama hiyo kwamba Aprili 3, 2016, katika Kata ya Nyangamala, Wilaya na Mkoa wa Lindi, washtakiwa hao walifanya mkusanyiko usio halali hivyo kuomba iwape adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwao na wengine.

Akizungumza nje ya Mahakama hiyo, wakili wa washtakiwa Deusdet Kamalamo alisema wanajiandaa kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

“Tutakata rufaa muda siyo mrefu leo (jana) ninaandaa barua ya kuomba hukumu ili tuanze kuandaa rufaa,” alisema Kamalamo.

Tarime

Huko Tarime, hakimu mkazi wa wilaya ya hiyo, Amon Kahimba alimhukumu Sanya pamoja na mtendaji wa Kata ya Nyangasaka, James John kila mmoja kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa mawili ambayo kila moja lilikuwa na adhabu yake.

John alifungwa baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ambayo kila moja lina adhabu yake. Katika kosa la kwanza, alihukumiwa faini ya Sh1milioni au kwenda jela miaka miwili na katika kosa la pili, alihukumiwa faini ya Sh1.5 milioni au kwenda jela miaka mitatu.

Kwa upande wa Sanya alihukumiwa kifungo cha miaka miwili bila faini na katika kosa la kwanza na la pili alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu, yote bila faini.

Awali, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara, Yahya Mwinyi alisema washtakiwa walitenda makosa hayo Aprili 2013, wakati huo Sanya akiwa ni Diwani wa Nyamagaro kabla ya kata hiyo kugawanywa.

Mwinyi alisema Sanya akiwa Mwenyekiti wa Maendeleo ya Kata (WDC) na John akiwa katibu, walibadilisha matokeo ya aliyekuwa mshindi nafasi ya mwakilishi mjumbe wa baraza la Katiba Wilaya ya Tarime, Juma Ally na kumpa Jomo Nyamulanga ambaye hakuwa mshindi.

Aliongeza kuwa viongozi hao wote walighushi nyaraka kinyume cha Sheria ya Takukuru na walitumia muhtasari wa uongo kubadilisha matokeo ya mshindi halali.

Mbowe atoa msimamo wa Chadema

Baada ya viongozi wake kadhaa kutiwa mbaroni, kushtakiwa na baadhi kuhukumiwa vifungo jela, uongozi wa Chadema umueagiza sensa ya nchi nzima kubaini wanachama, viongozi na wafuasi wake waliokamatwa, kushtakiwa na kufungwa jela kwa makosa yanayohusiana na shughuli za kisiasa.

Agizo hilo lilitolewa jana jijini Mwanza na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipokuwa akifungua mkutano wa uchaguzi Kanda ya Ziwa.

“Tukishapata orodha kamili tutautangazia umma ndani na nje ya nchi madhila yote ambayo viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wanakutana nayo,” alisema Mbowe. Alisema hukumu ya Mathew ya kifungo cha miezi minane jela bila faini kinafifisha nguvu ya vyama vya siasa.