Viroba kusafirishwa kwa ulinzi mkali wa polisi

Muktasari:

Tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotangaza kusitishwa kwa uzalishaji na matumizi ya viroba kuanzia Machi Mosi mwaka huu, wafanyabiashara mbalimbali walikamatwa wakiwa na shehena ya pombe hiyo.

Dodoma. Serikali imesema itaweka ulinzi mkali wa polisi wakati wa kusafirisha shehena ya pombe kali zilizofungashwa kwenye mifuko ya plastiki ‘viroba’, kuirudisha viwandani ili iwekwe kwenye chupa.

Tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotangaza kusitishwa kwa uzalishaji na matumizi ya viroba kuanzia Machi Mosi mwaka huu, wafanyabiashara mbalimbali walikamatwa wakiwa na shehena ya pombe hiyo.

Akizungumza juzi usiku bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage alisema kuwa uhamishaji wa bidhaa hiyo utalindwa vikali na kwamba wafanyabiashara waliokamatwa na pombe hiyo watalazimika kulipa gharama za kuisafirisha.

“Hatuwezi kumwaga kuku kwenye mtama. Maelekezo ndiyo hayo, kuna ulinzi mkali wa kutoa bidhaa kuipeleka kiwandani na tutasimamia vile viwanda vikitoa kwenye makaratasi kuweka kwenye chupa” alisema.

Wakati Bunge lilipoketi kama kamati ya matumizi ya Bunge zima, Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Anthony Komu alitishia kushika shilingi ya mshahara wa Waziri, endapo hatampa maelezo ya kutosha kwa vile suala hilo limewagharimu wengi.

“Ninachosema mimi baada ya marufuku hii, Serikali ilitoa maelekezo kwa wenye akiba ya ile pombe iliyopo kwenye hivyo vifungashio ifanyiwe stock taking (ihakikiwe) na polisi walifanya hivyo,” alisema Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi vijijini.

Kwa mujibu wa Komu, baada ya kufanyika hivyo, Serikali iliahidi kutoa maelekezo ili pombe hizo zikajazwe kwenye chupa, lakini hadi hiyo jana ilikuwa imepita miezi miwili bila maelekezo hayo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mwijage alisema kimsingi wazalishaji wote wanakubaliana na uamuzi wa Serikali kuzuia vifungashio hivyo na wameshapewa maelekezo ya hatua za kufanya.

Waziri Mwijage alisema mfanyabiashara yeyote ambaye bidhaa yake ilizuiliwa na iko kwenye maghala, aende kuonana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira.

“Vitoke kwenye karatasi viwekwe kwenye chupa ya lita moja, lita tano hata lita 10,” alisema Waziri Mwijage.

Hata hivyo, maelezo hayo yalionekana kutojibu swali lililohusu nani atabeba dhamana, hadi Naibu Spika, Tulia Ackson alipomkumbusha Waziri kuwa swali la Komu lilihusu gharama.

“Mheshimiwa Waziri, nadhani swali la mheshimiwa Komu ilikuwa kwamba gharama za kubadilisha sasa kutoka kwenye vifungashio vya karatasi kwenda kwenye chupa, nani anahusika? Alihoji Tulia.

Akijibu swali hilo, Waziri Mwijage alisema yeye ni Waziri hahusiki na mambo ya kiutendaji na ndiyo maana amewataka wafanyabiashara hao kuwasiliana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais.